IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu / 104

Sura Al-Humazah yataja moto unaosubiri wasengenyaji

15:27 - August 09, 2023
Habari ID: 3477404
TEHRAN (IQNA) – Baadhi ya watu hufikiri kwamba kwa sababu wako katika nafasi ya juu au wana hadhi fulani, wanaweza kuwadhihaki au kuwadhalilisha wengine.

Hata hivyo, wanapaswa kujua kwamba adhabu kali inawangoja, kwa mujibu wa Sura Al-Humazah.

Al-Humazah ni jina la sura ya 104 ya Qur'ani Tukufu ambayo ina aya 9 na iko katika Juzuu ya 30

Ni Makki na Sura ya 32 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume (SAW).

Neno Humazah linalokuja katika Aya ya kwanza linaipa Sura jina lake. Pia inaitwa Lumazah, neno lingine katika aya kwanza. Humazah na Lumazah ni maneno yanayorejelea wale wanaozungumza kuhusu kasoro za wengine na kujihusisha katika kusengenya.

Mwenyezi Mungu katika sura hii anawaonya wale wanaokusanya na kulimbikiza mali ili kupata ubora juu ya watu wengine kwamba watatupwa kwenye moto unaoteketeza.

Baadhi ya wafasiri wa Qur'ani Tukufu wanaamini kuwa Sura hii iliteremshwa kuhusu wale waliojihusisha katika kumkashifu na kumsengenya Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) au wale waliotaka kumkashifu.

Sura inatoa onyo kali kwa wale ambao wana shauku ya kukusanya na kujilimbikizia mali na wanataka kuwadhalilisha wengine kwa mali hii. Wanafikiri utajiri wao unawafanya kuwa wa milele lakini hiyo si kweli.

Sura inaanza na neno la indhari au onyo  (Ole wake), ambalo ni onyo kuu katika Qur'ani Tukufu. Na inahusu wale wanaokejeli, kuwatukana au kuwasengenya wengine.

Mwenyezi Mungu anasema watatupwa ndani ya al-Hutama: "Moto wa Mwenyezi Mungu ulio washwa. Ambao unapanda nyoyoni.  Hakika huo utafungiwa nao. Kwenye nguzo zilio nyooshwa.” ( Aya 6-9 ) )

Moto huo unaitwa Narullah (moto wa Mungu) ambao pengine ni kuonyesha jinsi ulivyo mkubwa.

Moto hupenya ndani ya mioyo yao na kuwameza kwa sababu wanaumiza mioyo ya wengine kwa maneno yao.

Neno Hutama linakuja katika Sura hii ya Qur'ani Tukufu pekee na linahusu moto ambao kwanza hupenya ndani ya nyoyo na kuunguza kutoka ndani kisha kuunguza nje ya mwili.

Habari zinazohusiana
captcha