IQNA

Watetezi wa Qur'ani Tukufu

Rais wa Venezuela awakosoa watawala wa Ulaya kwa kunyamazia kuvunjiwa heshima Qur'ani

21:48 - August 07, 2023
Habari ID: 3477392
TEHRAN (IQNA)- Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amewakosoa vikali watawala wan chi za Ulaya kutokana na ukimya wao kuhusu vitendo vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu nchini Uswidi na Denmark.

Katika mahojiano na mtandao wa habari wa televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon siku ya Jumatatu, Maduro amesema: "Ninalaani vitendo hivi vya kibaguzi vya chuki dhidi ya mataifa ya Kiislamu."

Kiongozi huyo wa Venezuela amesema: "Kimya cha viongozi wa Ulaya juu ya kuchomwa kwa nakala za Qur'ani kinashangaza, na kimya hicho ni sawa na kushiriki kwao katika uhalifu huo."

Maduro alisema haiwezekani kufumbia macho chokochoko hizo zinazodhalilisha Uislamu na wafuasi wake.

Rais wa Venezuela ameendelea kwa kuhoji hivi, "Je, Wakristo wa Ulaya wangesema nini ikiwa Biblia ilichomwa mbele yao?"

Rais wa Venezuela alisema ni "kawaida kabisa" kwamba jumuiya ya Kiislamu duniani ilionyesha "mtazamo wa hasira" kwa kudhalilishwa kwa kitabu hicho kitakatifu.

Katika muda wa wiki kadhaa zilizopita, Qur'ani Tukufu imekuwa ikikabiliwa na vitendo vya kuvunjiwa heshima na watu wenye misimamo mikali mara kadhaa nchini Uswidi na Denmark, huku serikali za nchi hizo zimeidhinisha na kuhalalisha vitendo hivyo viovu kuwa ni "uhuru wa kujieleza."

Vitendo hivyo vya dhidi ya Qur'ani Tukufu vimechochea hasira ya jamii nzima ya Waislamu duniani kote.

3484670

Habari zinazohusiana
captcha