IQNA

Katika kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu

Kuwait kuchapisha nakala laki moja za Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kiswidi

15:03 - July 12, 2023
Habari ID: 3477266
TEHRAN (IQNA)- Serikali ya Kuwait itasambaza nakala 100,000 za Qur'ani Tukufu nchini Uswidi zilizotarjumiwa kwa lugha ya Kiswidi.

Uamuzi huo umchukuliwa baada ya Salwan Momika, mkazi wa Uswidi, kurarua na kuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu katikati ya Stockholm mbele ya Msikiti Mkuu wa jiji hilo.

Momika alichagua kufanya kitendo hicho kiovu katika sikukuu ya Idul al-Adha, mojawapo ya sherehe muhimu za Kiislamu zinazoadhimishwa na Waislamu duniani kote.

Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Al-Qabas, shirika la kusimamia uchapishaji na usambazaji wa Qur'ani Tukufu nchini Kuwait limetangaza kwamba kwa mujibu wa amri ya Waziri Mkuu, Nawaf Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah, nakala 100,000 za Qur'ani kwa lugha ya Kiswidi zitachapishwa na kusambazwa katika miji ya Uswidi kwa uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kuwait.

Baraza la Mawaziri la Kuwait pia liliidhinisha suala hili katika kikao chake cha jana na kutangaza kwamba idadi hiyo ya nakala za Qur'ani Tukufu itachapishwa na kusambazwa ili kusisitiza moyo wa kustahamiliana na maelewano katika dini ya Uislamu, kulingania maadili ya Kiislamu na kuishi pamoja baina ya wanaadamu wote kwa amani.

Baada ya upinzani na hasira kubwa ya nchi za Kiislamu na kuongezeka mashinikizo na vitisho vya kimataifa, Waziri wa Sheria wa Uswidi Alkhamisi iliyopita (Julai 6) alikiri kwamba kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini nchini humo kumekuwa na madhara kwa usalama na amani na kutangaza kuwa suala la kuutambua uchomaji wa Qur'ani kuwa ni kosa la jinai linachunguzwa na kufanyiwa kazi.

Gunnar Stromer, Waziri wa Sheria wa serikali ya Uswidi amesema: "Kuchomwa moto Qur’ani katika siku za hivi karibuni (mjini Stockholm), kumeharibu usalama wa ndani wa Sweden.”

3484307

Habari zinazohusiana
Kishikizo: uswidi qurani tukufu
captcha