IQNA

Waislamu Denmark

Denmark Yakataa Mpango wa Kupiga Marufuku Hijabu Mashuleni

22:26 - March 03, 2023
Habari ID: 3476651
TEHRAN (IQNA) – Serikali ya Denmark inasema haitaunga mkono hoja inayotaka kupiga marufuku wanafunzi na wafanyakazi kuvaa hijabu katika shule za msingi.

Hayo yametangazwa na Waziri wa Uhamiaji wa Denmark Kaare Dybvad Bek akijibu pendekezo la chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Denmark People’s Party kwa ajili ya bunge kujadili kupiga marufuku vazi la hijabu shuleni.

Wakati Denmark inakabiliwa na "changamoto kubwa za udhibiti mbaya wa kijamii na ukandamizaji wa wasichana wadogo katika mazingira fulani", marufuku kama hayo yatakiuka sheria za Denmark, waziri alisema, The Local iliripoti.

"Ni tathmini ya kisheria kwamba pendekezo la kupiga marufuku hijabu za Kiislamu katika shule za msingi haliwezi kutekelezwa ndani ya mfumo wa Katiba na wajibu wa kimataifa wa Denmark," aliandika.

“Kwa hiyo, serikali haiwezi kuunga mkono pendekezo hilo. Lakini hata hivyo tutaendelea kupambana na shuruti na ukandamizaji unaohusiana na heshima na udhibiti mbaya wa kijamii,” waziri pia alisema.

Uamuzi huo sasa unatilia shaka msimamo wa serikali kuhusu mapendekezo ya Tume ya Denmark ya Mapambano ya Wanawake Waliosahaulika, chombo kilichoundwa na serikali ya zamani ya Denmark.

Kulingana na ripoti ya tume hiyo, "matumizi ya skafu katika shule ya msingi yanaweza kuleta mgawanyiko kati ya watoto katika makundi mawili - 'sisi' na 'wao'".

Pamoja na kupiga marufuku hijabu, tume hiyo ilitoa mapendekezo mengine ikiwa ni pamoja na kutoa kozi za lugha ya Kidenmaki, kukuza desturi za kisasa za malezi ya watoto katika familia za makabila madogo, na kuimarisha elimu ya ngono katika shule za msingi.

Pendekezo hili la kupiga marufuku hijabu limezua taharuki nchini Denmark, huku maelfu kadhaa ya watu wakijitokeza katika barabara ya Copenhagen kupinga pendekezo hilo.

Uislamu ndio dini kubwa zaidi ya walio wachache nchini Denmark. Kulingana na Ripoti ya Idadi ya Watu Ulimwenguni iliyochapishwa mnamo 2019, Waislamu 313,713 wanaishi Denmark, au takriban 5.40% ya idadi ya watu wote nchini humo.

Kuvaa hijabu ni wajibu kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu na hivyo vazi hilo haliwezi kutazamwa kama nembo tu ya kidini.

Katika kura ya maoni iliyofanywa na Voxmeter kwa niaba ya shirika la habari la Ritzau, 56.1 ya waliojibu walisema 'hapana' kwa kupiga marufuku vazi la hijabu shuleni.

Sehemu ndogo zaidi ya asilimia 28.2 walisema ‘ndiyo’ kwa marufuku hiyo huku asilimia 15.7 wakijibu ‘hawajui’.

3482680

Kishikizo: hijabu denmark waislamu
captcha