IQNA

Denmark yaruhusu dini kutusiwa, aliyevunjia Qur'ani heshima aachiliwa huru

12:11 - June 04, 2017
Habari ID: 3471006
TEHRAN (IQNA)-Denmark Imefuta sheria inayopiga marufuku kuzivunjia heshima dini na punde baada ya hapo aliyeivunjia heshima Qur'ani ameachiliwa huru.
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, siku ya Ijumaa Bunge la Denmark lilifuta sheria iliyopitishwa miaka 334 iliyopita inayopiga marufuku kuzivunjia heshima dini hadharani ikiwemo kuchoma moto Vitabu vitakatifu.

Wabunge wa bunge la Denmark walifuta kifungu cha 140 cha katiba ya nchi hiyo kinachoeleza kuwa mtu yeyote atakayetusi na kuvunjia heshima hadharani misingi  au matukufu ya wafuasi wa dini yoyote atatozwa faini ya fedha taslimu au kuhukumiwa kifungo cha miezi minne jela.

Bruno Jerup, mbunge aliyewasilisha hoja ya kufuta sheria hiyo amedai kuwa dini haipasi kuamuru kitu gani kinaruhusiwa na kitu gani ni marufuku kukisema hadharani, na kwamba eti sheria hiyo iliyofutwa inaipa dini upendeleo kamili katika jamii.

Punde baada ya kupitishwa sheria hiyo, raia wa Denmark ambaye amesambaza video yake katika Facebook akiteketeza Qur'ani Tukufu ameachiliwa huru na kesi yake kufutwa.

Mtu huyo mwenye umri wa miaka 42 ambaye jina lake halikutajwa alikuwa anatazamiwa kufungwa miezi mine jela kutokana na jinai yake hiyo mwaka 2015.

Itakumbukwa kuwa mnamo mwaka 1938, watu wanne walihukumiwa kwa kosa la kuonyesha hadharani mabango yenye maandishi yaliyo dhidi ya Mayahudi. Aidha mwaka 1946 watu kadhaa walihukumiwa kulipa faini baada ya kufanyia kejeli  ubatizo katika hadhara ya ugeni mjini Copenhagen.

Hata hivyo licha ya kuweko kwa miaka mingi sheria hiyo iliyofutwa Ijumaa ambayo ilikuwa inapiga marufuku kuvunjia heshima dini, serikali ya Denmark imefumbia macho mara kadhaa na kutowaadhibu watu ambao wameivunjia heshima Qur'ani Tukufu, Bwana Mtume Muhammad SAW na matukufu mengine ya Waislamu. Denmark ni kati ya nchi za Ulaya zenye idadi kubwa ya wanasiasa wenye chuki dhidi ya Uislamu.

3606206



captcha