IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Erdogan: Kuvunjiwa heshima Qur'ani nchini Uswidi ni dalili ya kiwango cha kutisha cha chuki dhidi ya Uislamu

15:25 - July 09, 2023
Habari ID: 3477260
ANKARA (IQNA)- Rais wa Uturuki amesema "Shambulizi la chuki dhidi ya kitabu chetu, Qur'ani, huko nchini Uswidi katika siku ya kwanza ya Sikukuu za Iddul Adh'ha, lilianika kiwango cha kutisha cha chuki dhidi ya Uislamu."

Rais Recep Tayyip Erdoganwa Uturuki amesema kuna haja kwa umma wa Kiislamu kuungana na kuwa na mshikamano, ili uweze kukabiliana na vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vilivyoshtadi katika nchi za Magharibi.

Aidha ameashiria vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na matukufu mengine ya kidini na kueleza kuwa, kitendo cha kuvunjiwa heshima kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu huko nchini Uswidi hivi karibuni hakikubaliki.

Amesisitiza kuwa: Sisi sote Waislamu tuna jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa vitendo vya aina hiyo, ambavyo tumevilaani vikali hapa Uturuki, havikaririwi popote pale duniani." 

Erdogan amebainisha kuwa, iwapo Waislamu wataungana na kushirikiana, na vile vile kuwa na moyo mmoja na kushikana mikono, hakuna mtu yeyote duniani atakuwa na uthubutu wa kuyavunjia heshima matukufu yao.

Rais wa Uturuki amewahutubu Wamagharibi na kuwaeleza bayana kuwa, ni unafiki kwa wao kuutumia uhuru wa maoni na kujieleza kama kibali na idhini ya vitendo vya fedheha vya kuvunjia heshima matukufu ya dini nyingine.

Waislamu kote duniani wamepaza sauti zao kulalamikia kitendo hicho kiovu cha kudhalilisha na kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini Sweden, huku kampeni kubwa ya dunia nzima ya kususia bidhaa zinazozalishwa na nchi hiyo ya Magharibi ikishika kasi.

3484262

captcha