IQNA

Wanazuoni Mashuhuri wa Kiislamu Duniani/2

Ufafanuzi wa Muhammad Sadiq Arjun wa Mbinu za Ufasiri

22:13 - October 14, 2022
Habari ID: 3475930
TEHRAN (IQNA) – Sheikh Muhammad Sadiq Ibrahim Arjun (1903- 1981) alikuwa mwanazuoni wa Al-Azhar ambaye kazi zake zilizoandikwa na kurekodiwa kuhusu tafsiri ya Quran ni vyanzo vyema vya utafiti katika nyanja Tafsiri ya Qur’ani Tukufu na sayansi za Kiislamu.

Moja ya vitabu vyake ni Al-Quran Al-Azim: Hidayat wa I’jaz fi Aqwal al-Mufasireen” (Qur’ani Tukufu: Mwongozo na Muujiza wake katika Maneno ya Wafasiri wa Qur’ani). Katika kitabu hiki, amezungumzia kwa ufupi mbinu zinazotumiwa na wafasiri katika zama tofauti na kazi zao katika uwanja huu wa sayansi za Kiislamu.

Anasema katika kitabu hicho wafasiri wamefanya juhudi za kila namna katika maandishi yao ili kufikisha elimu na mafundisho kwa jamii na kutumia chochote walichokuwa nacho kujifunza na kufanya utafiti wa tafsiri ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Anasisitiza kuwa Qur’ani Tukufu ni nuru na muongozo kwa wanadamu na inawalingania watu kwenye ukuaji na inawaongoza kwenye wokovu na furaha katika dunia hii na ijayo na hiyo ndiyo sababu ya kuwa ni kitabu cha milele kinachofungua upeo wa elimu na ufahamu.

Sheikh Arjun pia anasema katika kitabu chake kwamba muongozo wa Qur’ani Tukufu yenyewe ndio nguzo ya muujiza wa kiroho wa Kitabu Kitakatifu.

Aliandika kitabu kingine chenye jina la “Nahw Minhaj Li Tafseer al-Quran” (Mtazamo wa Tafsiri ya Qur’ani) ambamo anawataka watafiti wa masomo ya Qur’ani Tukufu kuchukua mbinu nzuri na sahihi kwa lengo la kufafanua muongozo wa Qur’ani Tukufu na aya zake kwa njia ambayo inathibitisha kudumu kwa Qur’ani Tukufu na hadhi yake kama kitabu cha wanadamu.

Katika kitabu hiki, mwanachuoni huyu wa Kimisri anaonya kuhusu mitazamo potofu ambayo inadhoofisha hadhi ya aya za Qur’ani Tukufu na kutoa tafsiri za kiholela ili kuwaridhisha baadhi.

Anawaalika wanazuoni kurejea kwenye mwongozo wa Mwenyezi Mungu wa Qur'an na kutoa utafiti wa Kiislamu-Qur’ani ambao unaunganisha zama za kisasa na miaka ya mwanzo baada ya ujio wa Uislamu.

Madhumuni yake katika kitabu hiki si kutambulisha mbinu za tafsiri ya Qur’ani kwa Waislamu bali ni kuiweka Quran katika hadhi inayostahiki katika masomo ya Kiislamu.

Sheikh Arjun anasisitiza kwamba Qur’ani Tukufu inabakia kuwa chanzo halisi cha sayansi na mafundisho ya Kiarabu, lakini wanachuoni na watafiti wa Umma wa Kiislamu hawajaizingatia ipasavyo.

captcha