IQNA

Kadhia ya Palestina

OIC yasisitiza Quds Tukufu ni sehemu isiyoweza kutenganishwa ya Palestina

18:22 - March 16, 2024
Habari ID: 3478525
IQNA- Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imesisitiza katika taarifa yake kwamba, mji wa Quds (Jerusalem) ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na ardhi ya Palestina na mji mkuu wa Dola ya Palestina, na eneo lote la Msikiti wa Al-Aqsa ni makhsusi kwa ajili ya ibada ya Waislamu tu.

Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na OIC ilisema, madhumuni ya hatua za utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuweka vizuizi vya chuma katika eneo la Msikiti wa Al-Aqsa na kuzuia uhuru wa kuingia mahala hapo patakatifu ni kutaka kubadilisha hadhi ya kisheria na kihistoria ya Msikiti wa Al-Aqsa, na kusisitiza kuwa vitendo hivi havikubaliki na vinalaaniwa vikali.

OIC imesema, shambulio dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa na hujuma dhidi ya waumini katika viwanja vya msikiti huo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa. Imesisitiza kuwa, hatua na maamuzi yote ya utawala ghasibu wa Israel yanayolenga kulazimisha mamlaka ya Israel huko Al-Quds na maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo, hususan Msikiti wa Al-Aqsa, ni kinyume cha sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala hilo na hayakubaliki.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imetilia mkazo ulazima wa kuheshimiwa maeneo matakatifu na uhuru wa kuabudu ndani ya maeneo hayo, na kusema utawala ghasibu wa Israel unabeba dhima kamili ya matokeo ya ukiukaji wa sheria katika Quds na Msikiti wa Al-Aqsa.

Vilevile OIC imeitaka jamii ya kimataifa itekeleze majukumu yake ili kukomesha ukiukaji huo wa sheria wa utawala wa Kizayuni, unaozidisha ghasia,  mivutano na kuvuruga usalama na katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Ijumaa ya jana askari wa utawala ghasibu wa Israel waliwazuia maelfu ya Waislamu kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa kutekeleza ibada ya Swala ya Ijumaa ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ndani ya msikiti huo.

Israel pia ilituma maelfu ya askari polisi katika eneo la zamani la mji wa Quds, karibu na Msikiti wa Al-Aqsa kwenye lango la kuingia kwenye eneo hilo takatifu.

3487591

captcha