IQNA

AI: Israel ni utawala wa Apathaidi (ubaguzi wa rangi)

15:59 - February 02, 2022
Habari ID: 3474881
TEHRAN (IQNA)- Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeutuhumu utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni utawala wa baguzi wa rangi wa apartheid. Amnesty Internation inakuwa taasisi ya karibuni zaidi ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kuitangaza Israel kuwa ni utawala wa apartheid.

Ripoti yenye karibu kurasa 300 ya Amnesty International iliyopewa anwani "Mfumo wa Israel wa kutawala kikatili na kawandamiza Wapalestina" iliyotolewa Jumanne ya jana inaeleza vitendo vya kinyama vya kuwalazimisha watu kuondoka katika makazi yao, kuwekwa kizuizini, mauaji ya kikatili na majeraha makubwa, kunyimwa haki za msingi na kuwakandamiza na kuwatesa Wapalestina, na kuonesha jinsi utawala huo ulivyoundwa kwa msingi wa dhulma na ukandamizaji wa kimfumo dhidi yaWapalestina. Ripoti hiyo imesema: "Amnesty International inaamini kuwa utawala wa Israel unawatambua Wapalestina kama kundi la watu wa chini wasio Wayahudi." Ripoti hiyo imesema: "Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1948, utawala wa Israel umetekeleza sera ya wazi ya kuanzisha na kuzidisha idadi ya jamii ya Kiyahudi na kudhibiti zaidi ardhi ya Palestina kwa ajili ya Mayahudi." 

Jamii ya kimataifa ichukue hatua dhidi ya Israel

Katibu Mkuu wa Amnesty International Agnès Callamard amesema: "Jamii ya kimataifa lazima ichukue hatua za kukomesha uhalifu huu. Hatua za utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina zinakiuka sheria za kimataifa."

Utawala wa Kizayuni wa Israel umekasirishwa sana na ripoti hiyo na kuitaja kuwa ni chuki dhidi ya Wayahudi. Israel imeitaja Ripoti ya Amnesty International kuwa "isiyo sahihi na yenye upendeleo" hata kabla ya kutolewa kwake rasmi.

Serikali ya Marekani pia imelaani ripoti ya Amnesty International kuhusu sera za ubaguzi wa rangi za utawala wa Kizayuni wa Israel. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Marekani, Ned Price amesema Washington inapinga mtazamo wowote unaoitambua Israel kuwa ni utawala wa ubaguzi wa rangi wa apartheid. Hatua ya Marekani ya kuutetea kwa nguvu zote utawala haramu wa Israel na hata kukana jinai na ubaguzi wa rangi unaofanywa na Israel ni kielelezo cha uhusiano wa tawala hizo mbili za kibeberu na jinsi Washington ilivyojitolea kwa hali na mali kuuhami utawala huo ghasibu na kandamizi dhidi ya Wapalestina. Ijapokuwa inasemekana kwamba serikali ya Joe Biden imeahidi kutilia maanani zaidi masuala ya haki za binadamu, lakini imebainika kuwa, ahadi hiyo huwa butu na ya hewa pale Israel inapofanya jinai za kutisha na kulaaniwa na jumuiya za kimataifa kama Amnesty International.

Ubaguzi wa rangi ni jinai dhidi ya binadamu

Sheria za kimataifa hususan mkataba wa Roma uliounda Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) zinautambua ubaguzi wa apartheid kuwa ni jinai dhidi ya binadamu. Kwa miongo kadhaa sasa Israel imekuwa ikitekeleza siasa za kuwatenganisha watu kwa mujibu wa kaumu na mbari zao na kuwabana Wapalestina katika sehemu moja ya ardhi kupitia njia ya kujenga ukuta unaotenganisha baina ya maeneo ya Wapalestina na Wayahudi hususan katika ardhi za Palestina zilizokaliwa kwa mabavu mwaka 1967. Utawala wa Kizayuni pia unawabagua kimfumo Wapalestina, na hali hii inashuhudiwa zaidi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ukiwemo Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Hapana shaka kuwa, ukatili na vitendo vya kinyama vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina haviishii kwenye ubaguzi wa rangi bali utawala huo unaendelea kunyakua ardhi zao katika maeneo tofauti ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi na kuwapa makazi humo Wazayuni zaidi. Sambamba na hayo Israel imekuwa ikifanya mashambulizi ya kikatili katika Ukanda wa Gaza, kuwaua Wapalestina na kuharibu miundombinu na makazi yao, na inalizingira eneo hilo lenye wakazi wengi wa Palestina tangu mwaka 2007. Hatua hizi za Israel ni kielelezo cha wazi cha uhalifu na jinai dhidi ya binadamu.

3477645

captcha