IQNA

Chama cha Leba Uingereza chatangaza Israel ni utawala wa kibaguzi wa Apathaidi

21:05 - September 27, 2021
Habari ID: 3474349
TEHRAN (IQNA)- Mkutano mkuu wa chama cha Leba nchini Uingereza umepigia kura na kupitisha hoja ya kuitambua Israel kuwa ni utawala unaotenda jinai ya ubaguzi wa Apathaidi, na kukifanya kuwa chama cha kwanza kikubwa cha siasa barani Ulaya kuchukua msimamo huo dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni.

Kupitishwa hoja hiyo kunakipa jukumu chama hicho la kutekeleza vikwazo, ikiwemo kusimamisha biashara ya mauzo ya silaha kati ya Uingereza na Israel na kutofanya miamala ya biashara na vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni.

Mswada wa hoja hiyo umesema: "mkutano unalaani Nakba inayoendelea Palestina, ukatili wa kijeshi wa Israel wa kuushambulia msikiti wa Al Aqsa, uhamishaji watu kwa nguvu katika eneo la Sheikh Jarrah na shambulio lililosababisha vifo katika Ukanda wa Gaza."

Hoja hiyo iliyopitishwa na chama hicho kikongwe cha siasa nchini Uingereza imeashiria ripoti za mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch na B'Tselem ambayo mapema mwaka huu yalitoa hitimisho la kihistoria la kwamba Israel inatekeleza jinai ya ubaguzi aina ya Apathaidi kama ulivyotafsiriwa na Umoja wa Mataifa. 

Ripoti za mashirika hayo ya kutetea haki za binadamu zilibainisha jinsi ukatili wa kimpangilio unaofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina ulivyofikia kiwango cha kuwa jinai ya apathaidi.

Hitimisho la Human Rights Watch B'Tselem lilitokana na matokeo ya uchunguzi uliofanywa na Umoja wa Mataifa, wataalamu mashuhuri katika sheria za kimataifa na mabalozi wawili wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Katika hoja yake hiyo, chama cha Leba cha nchini Uingereza kimekaribisha pia uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC wa kufanya uchunguzi wa uhalifu uliofanywa tokea mwaka 2014 katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hata hivyo licha ya kupitishwa hoja hiyo na mkutano wa chama, bado haijafahamika uongozi wa Leba utachukua hatua gani kuhusiana na mwito huo uliotolewa na wanachama wa chama hicho.

Kiongozi wa chama cha Leba Keir Starmer amekuwa akivutana vikali na wanachama wa chama hicho wanaounga mkono utekelezaji wa sheria za kimataifa kuhusiana na haki za watu wa Palestina.

3475808

captcha