IQNA

Watetezi wa Qur'ani Tukufu

Al Azhar yapongeza marufuku ya vitendo ya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu nchini Denmark

14:16 - December 11, 2023
Habari ID: 3478021
IQNA - Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri kimepongeza hatua ya Denmark ya kupiga marufuku vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini humo na kutarajia nchi nyingine za Ulaya zitafanya hivyo.

Katika taarifa yake siku ya Jumamosi, Al-Azhar ilikaribisha sheria iliyopitishwa hivi majuzi na Bunge la Denmark kwamba ni haramu kuchoma moto nakala za Qur'ani Tukufu - tukio ambalo limetokea mara kwa mara katika nchi za Magharibi, ikiwa ni pamoja na Denmark.

Al-Azhar imesifu hatua hiyo kama "ya kupongezwa ", na kuongeza kwamba itazuia majaribio ya kukiuka na kushambulia matakatifu ya Waislamu.

Pia imesema sheria hiyo kama hatua ya kupunguza makali ya matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu na hivyo kukuza uraia mwema, amani ya jamii, na amani ya dunia, iliongeza taarifa hiyo.

Al-Azhar ilieleza matumaini yake kwamba hatua hiyo itazihimiza nchi nyingine za Ulaya ambazo zimeshuhudia matukio sawa na hayo kutunga sheria inayokataza kutukanwa dini na matukufu ya kidini.

Wizara ya mambo ya nje ya Qatar pia ilipongeza bunge la Denmark kwa kupitisha sheria hiyo siku ya Alhamisi na kuelezea matumaini ya kupunguzwa kwa matamshi ya chuki, haswa, chuki dhidi ya Uislamu.

"Wizara ya Mambo ya Nje inaeleza shukrani za Qatar kwa jibu la Bunge la Denmark kwa wito wa kuzuia kuchomwa kwa Qur'ani Tukufu. Wakati huo huo, inatarajia kupitisha sheria kama hizo kutoka kwa mabunge ya nchi ambazo zimeshuhudia kuchomwa kwa nakala za Qur'ani Tukufu," taarifa ya wizara hiyo ilisoma.

"Hii itachangia kukomesha uhalifu unaochochea chuki, ghasia na kutishia kuishi pamoja kwa amani wananchi."

Hivi karibuni, Denmark na Uswidi zimekuwa sehemu ya maandamano ambayo yalishuhudia uchomaji wa nakala za Qur'ani, ambayo mashuhuri zaidi yalifanyika mnamo Julai mbele ya balozi za Kiislamu na Kiarabu nchini Denmark.

Vitendo kadhaa vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu nchini Denmark miezi ya hivi karibuni vimezuia hasira miongoni mwa Waislamu katika majira ya kiangazi.

Sheria hiyo ya Denmark ya kupiga marufuku vitendo vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu ilipitishwa Alhamisi na inakataza "vitendo visivyofaa kwa maandishi yenye umuhimu mkubwa wa kidini kwa jumuiya ya kidini inayotambulika."

Muswada wa sheria hiyo ulilipitishwa kwa kura 94 za ndio na 77 za la katika bunge hilo lenye viti 179.

Uswidi pia inazingatia jinsi ya kukabiliana na vitendo vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu, lakini inachukua mtazamo tofauti na Denmark. Inachunguza uwezekano wa kuruhusu polisi kuzingatia usalama wa taifa wakati wa kuamua kuhusu maombi ya maandamano ya umma.

Vitendo vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu barani Ulaya vimeibua hasira duniani na kupelekea Waislamu waanzishe kampeni kubwa ya kiuchumi ya kususia bidhaa za nchi husika hasa Uswidi, Denmark na Uholanzi jambo ambalo limepelekea mashirika ya kibiashara ya nchi hizo kupata hasara kubwa.

 

captcha