IQNA

Jaribio la kumuua waziri mkuu wa Iraq kwa kutumia drone

20:51 - November 07, 2021
Habari ID: 3474526
TEHRAN (IQNA)- Rais Barham Salih wa Iraq amelaani jaribio la mauaji dhidi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mustafa al-Kadhimi.

Katika taarifa aliyotoa leo kupitia mitandao ya kijamii, Rais wa Iraq amesema, jaribio hilo la mauaji lililomlenga al Kadhimi ni njama ya kigaidi na jinai inayopasa kulaaniwa.

Halikadhalika Salih ametilia mkazo udharura wa kuwepo msimamo mmoja wa kukabiliana na watu wanaoinyemelea kwa nia ya kuivuruga amani na usalama wa Iraq na watu wake.

Rais Barham Salih amesisitiza kwa kusema: "haitawezekana kukubali hali ya mchafukoge na mapinduzi ya kijeshi yatawale mfumo wa sheria wa Iraq."

Vyombo vya usalama vya Iraq leo asubuhi vilitoa taarifa na kueleza kwamba limefanyika shambulio la kutaka kumuua Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mustafa al-Kadhimi. 

Kwa mujibu wa duru hizo, ndege zisizo za rubani au drone zilizosheheni mada za miripuko zililenga makazi ya kiongozi huyo katika mji mkuu Baghdad.

Al-Kadhimi alinusurika katika njama hiyo ya kutaka kumuua bila kujeruhiwa lakini duru za usalama zimesemam walinzi wasiopungua sita wa timu ya ulinzi ya kiongozi huyo walijeruhiwa katika hujuma hiyo ya leo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq Saad Maan amesema, vikosi vya usalama vilizitungua droni mbili, lakini ya tatu ilifanikiwa kuilenga nyumba ya waziri mkuu iliyoko kwenye eneo lenye ulinzi mkali la Ukanda wa Kijani yalipo pia majengo ya serikali na balozi za kigeni.

Akizungumza baada ya jaribio hilo la kutaka kumuua, Mustafa al-Kadhimi amesema: "Niko vizuri alhamdulillah na ninatoa wito wa kuwa na utulivu na uvumilivu kwa kila mtu kwa ajili ya maslahi ya Iraq."

4011160

captcha