IQNA

Katika Mkutano wa Rais wa Iran na Waziri Mkuu wa Iraq

Kuondolewa viza baina ya raia wa Iran na Iraq ni habari nzuri aliyokuja nayo Waziri Mkuu wa Iraq

21:36 - September 12, 2021
Habari ID: 3474287
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo na waandishi wa habari akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Iraq kwamba, idadi ya wafanya ziara wa Iran katika Arubaini ya Imam Husain AS itaongezwa mwaka huu.

Rais Ebrahim Raisi amesema hayo leo mbele ya waandishi wa habari hapa mjini Tehran akiwa pamoja Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al Kadhimi, na kuongeza kuwa, uhusiano wa Iran na nchi rafiki na ndugu ya Iraq ni mzuri sana na kwamba uhusiano huo umestawi katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni na unaweza kustawi zaidi na zaidi.

Amesema, kuondolewa viza baina ya raia wa nchi hizi mbili ni habari nzuri ambayo Waziri Mkuu wa Iraq ameitaarifu Iran.

Rais Raisi ameongeza kuwa, uhusiano mkubwa na uliokita mizizi vizuri; wa Tehran na Baghdad chimbuko lake ni imani na nyoyo za wananchi wa mataifa haya mawili na serikali zao.

Amesema, kuimarika uhusiano wa Iran na Iraq hakuzinufaishi tu nchi hizi mbili ndugu, lakini pia kuna mchango mkubwa wa kieneo na kimataifa na nchi hizi zinaweza kushirikiana zaidi na zaidi katika mahusiano ya kieneo na kimataifa.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Iraq amesema kwenye mazungumzo hayo na waandishi wa habari kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeisaidia sana Iraq kupambana na magaidi wa Daesh (ISIS) na kwa mara nyingine anawasilisha tena shukrani za wananchi wa Iraq kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Pia amesema, hii ni mara ya pili kutembelea Iran akiwa Waziri Mkuu wa Iraq na hilo pekee ni uthibitisho wa umuhimu mkubwa wa kuimarishwa zaidi na zaidi uhusiano wa nchi hizi mbili ndugu.

/3997006

captcha