IQNA

Taliban yaunda serikali ya mpito nchini Afghanistan

13:31 - September 08, 2021
Habari ID: 3474271
TEHRAN (IQNA)- Kundi la Taliban limetangaza kuunda serikali ya mpito ya Afghanistan huku kukiwa na maandamano dhidi ya kundi hilo mjini Kabul.

Kwa mujibu wa taarifa, kiongozi mwandamizi wa kundi hilo Mullah Mohammad Hassan Akhund ametangazwa mkuu wa serikali. Tangazo hilo la Jumanne limejiri wiki chache tangu Taliban ilipochukua madaraka baada ya kuteka aghalabu ya maeneo ya nchi hiyo na hatimaye Rais Ashraf Ghani kutoroka nchi.

Msemaji wa kundi hilo Zabiullah Mujahid amewaambia waandishi wa habari mjini Kabul kwamba Mullah Mohammad Hassan Akhund, ambaye alikuwa waziri wa ngazi ya juu katika utawala wa zamani wa Taliban katika miaka ya 1990, ndiye ameteuliwa kuwa waziri mkuu.

Hassan Akhund ni miongoni mwa watu ambao wamewekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa 

Kundi la Taliban liliahidi kuunda serikali itakayojumuisha kila jamii nchini humo, lakini nyadhifa zote za juu zimekabidhiwa viongozi wakuu wa vuguvugu hilo na mtandao wa Haqqani ambao ni tawi la Taliban na hufahamika kutokana mashambulizi yake ya kikatili.

"Tutajaribu kujumuisha watu kutoka maeneo mengine ya nchi. Hii bado ni serikali ya mpito,” amesema Zabiullah Mujahid.

Muda mfupi tu baada ya majina ya maafisa wa serikali mpya kutangazwa, Hibatullah Akhundzada ambaye ni kiongozi mkuu wa Taliban ambaye hajawahi kuonekana hadharani, alitoa taarifa iliyoitaka serikali mpya kufanya bidii katika kuzingatia na kulinda sheria za Kiislamu na kutii Sharia.

Lakini wakati Taliban linapojibadilisha kutoka kundi la kivita na kuwa kundi la kiutawala, maafisa wake wa usalama wanakabiliwa na ongezeko la maandamano yanayopinga utawala huo. Watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano hayo katika mji wa Herat magharibi mwa nchi hiyo.

Hayo yanajiri mnamo wakati shirika la Misaada la Umoja wa Mataifa OCHA, likitoa wito wa mchango wa dharura wa zaidi ya dola milioni 600 kusaidia katika utoaji misaada Afghanistan.

Msemaji wa shirika hilo Jens Laerke amesema huduma za msingi nchini Afghanistan zinaporomoka huku vyakula na misaada mingine ya kuokoa maisha ikikaribia kuisha.

Kulingana na Laerke, zaidi ya wanawake na watoto milioni moja nchini Afghanistan tayari wanakabiliwa na utapiamlo uliokithiri.

Jumapili tarehe 15 mwezi uliopita wa Agosti serikali ya Rais Muhammad Ashraf Ghani ilisambaratika na kiongozi huyo kuikimbia nchi baada ya Taliban kuingia Kabul mji mkuu wa Afghanistan. Hatua ya wanamgambo wa Taliban ya kuudhibiti mji wa Kabul imehitimisha uvamizi wa miaka 20 wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa kisingizio cha kuijenga upya Afghanistan.  Wananchi wa Afghanistan wanaamini kuwa, hali ya sasa ya nchi hiyo ni matokeo ya siasa zilizofeli za Marekani na waitifaki wake nchini humo.

3475657

Kishikizo: taliban afghanistan
captcha