Katika taarifa yake siku ya Jumatano, Al-Azhar imetoa wito kwa watu Waislamu kote duniani hasa katika nchi za Kiarabu na Kiislamu "kususia bidhaa zote za Uholanzi na Uswidi na kuchukua msimamo thabiti na wa umoja wa kuunga mkono Qur’ani yetu Tukufu, Maandiko Matakatifu ya Waislamu. Hii itakuwa ni hatua muafaka ya kutoa jibu kwa serikali za nchi hizi mbili, ambazo zimewaudhi Waislamu bilioni 1.5.”
Siku ya Jumapili, Edwin Wagensveld, mwanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Uholanzi, na kiongozi wa kundi la chuki dhidi ya Uislamu la Pegida, alirarua kurasa za Qur’ani Tukufu huko The Hague, mji mkuu wa Uholanzi. Video ya Wagensveld kwenye Twitter ilionyesha kuwa alichoma kurasa zilizochanwa za Qur’ani Tukufu
Uchochezi huo mpya ulifuatia kitendo sawa na hicho cha chuki dhidi ya Uislamu siku ya Jumamosi nchini Uswidi, ambapo mtu mwenye msimamo mkali raia wa Denmark alichoma nakala ya Qur’ani Tukufu mbele ya Ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm, katika kitendo ambacho kiliidinishwa na kusimamiwa na polisi nchini humo.
Taarifa ya Al Azhar imesema, "Wamevuka mipaka katika kulinda uhalifu wa kikatili na wa kinyama unaofanywa chini ya bendera maalum ya kinyama na iliyo dhidi ya maadili ya kile kinachojulikana kama 'uhuru wa kujieleza'.
Al Azhar imetoa wito kwa Waarabu na Waislamu wote "kushikamana na kususia, na kuwaelimisha watoto, vijana na wanawake kuhusu hilo."
Aidha Al Azhar imesema, "Wapotovu hawa hawatathamini kamwe thamani ya dini - ambayo hawajui chochote kuihusu – na hawawezi kusitisha wayatendayo isipokuwa tu pale watakapokabiliana na changamoto za za kifedha na kiuchumi. Hiyo ndiyo lugha pekee wanayoijua.”
Kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu kumezusha dhoruba ya lawama kutoka katika ulimwengu wa Kiislamu.