IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Msikiti New York washambuliwa na wenye chuki dhidi ya Uislamu

23:01 - July 13, 2022
Habari ID: 3475498
TEHRAN (IQNA) – Watu wawili walirusha kitu kinachofanana na bomu la molotov kwenye nembo kubwa ya hilali nje ya Msikiti wa Fatima al-Zahra huko Long Island, New York, Marekani siku chache kabla ya sherehe ya Kiislamu ya Idul Adha.

Mamlaka za mitaa sasa zinachukulia tukio hilo kama uhalifu wa chuki dhidi ya Uislamu.

Tarehe 3 Julai, imamu wa msikiti huo, Ahmed Ibrahim, alisikia mlipuko mkubwa kisha akaona miali ya moto. Jirani  mmoja alikuja mbio kusaidia kuzima moto.

Hakuna aliyejeruhiwa lakini baadaye ilibainika kuwa kifaa kilichowashwa kilitupwa kimakusudi katika eneo la jumla la msikiti au hasa kwenye alama ya mwezi mpevu.

"Hawakufanikiwa chochote lakini walionyesha chuki. Kwa nini?” Ibrahim alisema katika mkutano na waandishi wa habari siku chache baada ya tukio hilo.

Asiya, ambaye alitaka tu kutumia jina lake la kwanza, ni mkazi wa Ronkonkoma, kitongoji ambacho kisa hicho kilitokea. Alisema kuwa mashambulizi ya moto yameiacha jamii ikiwa na wasiwasi.

"Tunajua kilichotokea huko Christchurch ( New Zealand) ambapo Waislamu hao wote waliuawa ndani ya msikiti wao. Siwezi kusaidia lakini kujiuliza ikiwa tukio kama hilo litatokea hapa. Je, sisi tutalengwa?"

Kulingana na Afaf Nasher, mkurugenzi mtendaji katika Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR)- New York, hii ni mara ya kwanza kwa msikiti huo kukumbwa na tukio la aina hii.

"Bomu la moto ambalo lililipuliwa tarehe 4 Julai katika Masjid Fatima Al-Zahra linaweza kuwa liliharibu mali, lakini lilishindwa kuvuruga uimara wa jumuiya ya Kiislamu," Nasher alisema.

Gavana wa New York Kathy Hochul alitembelea msikiti huo siku ya Alhamisi na kusema: "(Vitendo hivi) vitaendelea, lakini tutaendelea kuinuka. Siwezi kuzuia chuki iliyo moyoni mwa mtu, lakini naweza kupitisha sheria kali."

"Jambo la msingi ni kwamba jumuiya hii ina umoja na nguvu zaidi kuliko hapo awali," alisema. "Hicho ndicho mhalifu huyu alitimiza."

Nayo Jumuiya ya Mayahudi Marekani imezindua mchango kwa njia ya intaneti na kuweza kuchanga dola elfu moja ambazo zitatumika kukarabati hilali iliyohairbiwa.

Idara ya polisi pia inatoa zawadi ya pesa taslimu ya hadi US$5,000 kwa habari zitakazopelekea kukamatwa mhusika au wahusika wa tukio hilo, ambalo linachunguzwa kama uhalifu wa chuki.

"Uhalifu wa chuki inayolenga jamii ya Kiislamu ni uhalifu wa chuki kwa wakazi wote wa Kaunti ya Suffolk," Kamishna wa Polisi wa Kaunti ya Suffolk Rodney Harrison alisema katika msikiti huo siku ya Jumanne. "Hili ni jambo ambalo kila mtu anapaswa kukasirika."

3479671

Habari zinazohusiana
captcha