IQNA

Wapalestina walaani kikao cha nchi nne za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel

21:06 - March 28, 2022
Habari ID: 3475084
TEHRAN (IQNA)- Harakati za Palestina za Hamas na Jihad ya Kiislamu zimelaani mkutano waliofanya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi nne za Kiarabu na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Naqab.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi nne za Kiarabu za Misri, Imarati au UAEA, Bahrain na Morocco jana walishiriki katika mkutano maalumu uliohudhuriwa na waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni Yair Lapid na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu la Naqab.

Katika mahojiano na chaneli ya Falastinul-Yawm, Daud Shahab, kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Jihadi ya Kiislamu ya Palestina amelaani hatua ya mawaziri hao wa nchi za Kiarabu ya kuhudhuria mkutano huo, akiutaja kuwa moja ya nembo za mapatano na ushirikiano unaounufaisha utawala ghasibu wa Kizayuni na sera zake za kivamizi; na kulilenga taifa la Palestina na ardhi yake.

Shahab amebainisha kuwa, mkutano huo wa kuuunga mkono utawala wa Kizayuni umefanyika ilhali ripoti za Umoja wa Mataifa zinasisitiza kwa uwazi kabisa kwamba jinai zinazofanywa na utawala huo ni za ubaguzi wa rangi na uangamizaji wa kizazi.

Wakati huohuo, Harakati ya Hamas nayo pia imelaani kufanyika mkutano huo wa Naqab na kusisitiza kuwa mkutano huo unaunufaisha utawala ghasibu tu; na mwenendo wa mawaziri wa mambo ya nje wa Kiarabu unagongana waziwazi na maslahi na misimamo ya umma wa Waarabu ya kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Mkutano wa Naqab unafanyika huku utawala ghasibu wa Kizayuni ukiwa unaendeleza ujenzi haramu wa vitongoji katika eneo hilo unalolikalia kwa mabavu.

Siku ya Jumanne iliyopita pia kilifanyika kikao cha pande tatu baina ya Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri, mrithi wa utawala wa Abu Dhabi Mohammad Bin Zayed al Nahyan na waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Naftali Bennett, katika eneo la kitalii la Sharm-Sheikh nchini Misri.

Mwaka 2020, Imarati na Bahrain zilisaini mkataba wa mapatano na utawala haramu wa Israel chini ya usimamizi wa Marekani.

3478287

captcha