IQNA

Askari wa Nigeria waua Waislamu 8 waliokuwa wakishiriki katika matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein AS

21:47 - September 29, 2021
Habari ID: 3474361
Polisi Nigeria jana Jumanne iliwashambulia waombolezaji waliokuwa katika marasimu ya siku ya arobaini ya mjukuu wa Mtume wa Uislamu, Imam Hussein AS na kuuwa shahidi Waislamu wasiopungua wanane.

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky, jana usiku ilitangaza kuwa askari usalama wa nchi hiyo wamewafyatulia risasi waombolezaji waliokuwa wamekusanyika katika marasimu ya  arobaini ya Imam Hussein A.S huko Abuja mji mkuu wa nchi hiyo. Abdullah Muhammad mwakilishi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ameeleza kuwa, waombolezaji katika marasimu hayo ya arobaini walikuwa wakielekea kwa amani katika barabara ya Abuja -Kubwa wakati walipofyatuliwa risasi na polisi. 

Ameongeza kuwa, waombolezaji wasiopungua 8 wameuawa shahidi na makumi ya wengine wamejeruhiwa. Waombolezaji wawilili waliuawa na polisi katika marasimu ya Ashura ya Imam Hussein A.S  nchini Nigeria na wengine kadhaa kujeruhiwa. Itakumbukwa kuwa, jeshi na polisi ya Nigeria tarehe 13 Disemba mwaka 2015 zilitekeleza mashambulizi makubwa katika husseiniya ya Baqiatullah katika mji wa Zaria jimboni Kaduna na kuwauwa shahidi mamia ya waombolezaji wa Waislamu wa Kishia waliokuwa wamekusanyika hapo  wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Ibrahim Zakzaky kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.  

Maadhimisho siku ya Arubaini (Arobaini au Arbaeen) hufanyika kila mwaka tarehe 20 Safar, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria, baada ya kupita siku Arobaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram, kwa ajili ya kukumbuka siku aliyouawa shahidi mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein AS na masahaba zake ambao walijitolea roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika jangwa la Karbala mwaka 61 Hijria Qamaria. Haram Takatifu ya Imam Hussein AS iko katika mji huo wa Karbala.

3475832

captcha