IQNA

Hamas yawasisitizia Wapalestina kuhusu kuendeleza mapambano dhidi ya Wazayuni

22:35 - July 11, 2021
Habari ID: 3474092
TEHRAN (IQNA)-Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imewataka wakazi wa Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan kudumisha mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kuhakikisha kwamba ardhi ya Palestina inakuwa kaa la moto kwa maghasibu hao.

Abdul-Latif al-Qanui amewataka Wapalestina wote wakazi wa Ukingo wa Magharibi kutoa jibu kwa jinai na uhalifu unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Al-Qanui amesema, wakazi wa Ukingo wa Magharibi wanapaswa kujibu ipasavyo uhalifu unaoendelea kufanywa na Israel na walowezi wa Kiyahudi kwa kuhakikisha kwamba, ardhi ya Palestina inakuwa kaa la moto kwa wavamizi hao na kukabiliana nao popote pale wanapokuwa. 

Msemaji wa Hamas amepongeza mapambano na kusimama kidete kwa Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi hususan wakazi wa maeneo ya Bita, Beit Dajan, Kafr Qaddum na Qasra mbele ya hujuma na uhalifu wa Israel na kusema kuwa, kuendelezwa maandamano dhidi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi ya Palestina kutakwamisha miradi ya kikoloni na utawala huo ghasibu.

Siku chache zilizopita walowezi wa Kizayuni walivamia kitongoji cha Jabal Sabih katika eneo la Bita kwa shabaha ya kujenga vitongoji zaidi vya walowezi, lakini Wapalestina walikwamisha mpango huo na kuwalazimisha kuondoka eneo hilo kwa kufanya maandamano makubwa na kupambana na wavamizi hao. 

Mamlaka ya Ndani ya Palestina yataka mazungumzo na Wazayuni

Wakati huo huo, Baadhi ya duru za Kizayuni zimetangaza kuwa Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ametoa masharti 14 ambayo ametaka yatekelezwe ili awe tayari kurudi tena kwenye meza ya mazungumzo ya mapatano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Gazeti la Raayul-Yaum limeandika kuwa, kanali ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni imetangaza kwamba, wiki hii, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina atakabidhi kwa serikali ya rais Joe Biden wa Marekani orodha ya masharti anayotaka yatekelezwe ili awe tayari kufanya tena mazungumzo ya mapatano na utawala huo haramu.

تأکید سخنگوی حماس مقابله مستمر با اشغالگران/ تلاش دولت خودگردان برای از سرگیری مذاکرات با اسرائیل

Televisheni hiyo ya utawala wa Kizayuni imedai kuwa, orodha hiyo inajumuisha masharti 14, ambayo yote yanalihusu eneo la Ufukwe  wa Magharibi na wala hayajagusia chochote kuhusu eneo la Ukanda wa Gaza.

Kufunguliwa tena mji wa Baitul Muqaddas pamoja na mashirika ya Kipalestina ambayo yalifungiwa shughuli zao katika mji huo tangu mwaka 2001, kurejea msikiti wa Al Aqsa kwenye hali na mazingira yake ya zamani, kusitisha kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa Quds katika majumba yao, kuachiwa huru idadi kadhaa ya mateka Wapalestina, kusimamishwa upanuzi wa vitongoji ukiwemo ujenzi wa vitongoji hivyo katika mji wa Baitul Muqaddas na kuwahamisha walowezi wote wa Kizayuni katika vitongoji vilivyojengwa kinyume cha sheria katika ardhi za Palestina, ni miongoni mwa masharti aliyotoa Mahmoud Abbas kwa ajili ya kufanya tena mazungumzo ya mapatano na utawala wa Kizayuni. 

Mazungumzo ya mapatano kati ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na Mamlaka ya Ndani ya Palestina yamesita tangu mwaka 2014 baada ya utawala huo ghasibu kukataa kuwaachia huru mateka unaowashikilia kwa miaka mingi na kutokubali kusimamisha ujenzi wa vitongoji katika Ufukwe wa Magharibi.

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amenukuliwa hapo kabla akisema: "tuko tayari kuhudhuria mazungumzo ya mapatano chini ya usimamizi wa kamati ya kimataifa ya pande nne; na tunakaribisha pia endapo itawezekana nchi zingine kushiriki katika mazungumzo hayo".

3983393

Kishikizo: hamas palestina wazayuni
captcha