Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo Jumamosi mjini Tehran aliponana na majimui
ya familia za mashahidi zikiwemo familia za mashahidi wa tarehe Saba Tir (Juni
28) na familia za mashahidi wanaolinda Haram. Sambamba na kuwaenzi mashahidi
kutokana na imani, jihadi, uongofu na maarifa yao aali na matukufu pamoja na
subira na kutotetereka familia za mashahidi hao amesema kuwa, mashahidi na
familia zao ni misingi na nguzo za nguvu na uwezo na uimara wa mfumo wa Jamhuri
ya Kiislamu ya Iran. Amesisitiza kuwa: Njia pekee ya kuweza Iran ya Kiislamu
kupiga hatua za kimaendeleo katika kila uwanja ni kuhuishwa roho ya kimapinduzi
ya wanajihadi wake.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ametoa mkono wa pole kwa
kukumbuka siku za kuuawa shahidi Amirul Muminin Imam Ali (Alayhis Salaam) na
kusema kuwa, mtukufu huyo ni shahidi mkubwa zaidi katika historia ya mwanadamu,
ni shahidi wa mihrabu na ni shahidi wa njia ya haki, ya istikama na ya
kutotetereka. Baada ya hapo ameashiria namna ilivyopita miaka 35 tangu
ulipotokea mripuko wa bomu katika ofisi ya chama cha Jamhuri ya Kiislamu hapo
tarehe Saba Tir 1360 (Juni 28, 1981) na kusema kuwa, waliofanya shambulio huo
ni genge khabithi la kigaidi ambalo halikuwa na chembe ya huruma na kwamba
wanachama wa genge hilo la kiafiriti baada ya kutoroka nchini Iran, kwa miaka
mingi wanaishi chini ya himaya ya nchi za Ulaya na Marekani zinazojigamba kuwa
ni viranja wa kupambana na ugaidi na watetezi wakuu wa haki za binadamu
duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, suala hilo ni kashfa
kubwa ya kihistoria kwa nchi za Ulaya na Marekani na kuongeza kwamba: Wanachama
wa genge hilo la kigaidi ni watu ambao walianzisha mashambulizi yao makali kwa
madai ya kuwahami wananchi bali hata kuulinda Uislamu lakini kadiri siku
zilivyopita ndivyo walivyofanya jinai kubwa kama vile mashambulizi ya tarehe
Saba Tir (Juni 28) na kuwaua kigaidi wananchi wa kawaida na hatimaye
kushirikiana na watu kama Saddam (kufanya mashambulizi dhidi ya wananchi wa
Iran na hata wa Iraq) na hivi sasa wanaungwa mkono kikamilifu na Marekani.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja shambulio la bomu la Juni 28, 1981 nchini
Iran kuwa ni tukio kubwa lenye masomo na ibra za kila namna na huku akielezea
masikitiko yake kutokana na kutofanyika juhudi za kutosha za kuyatangaza na
kuwaelimisha vijana matukio muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu na masuala
yanayohusiana na mashahidi, amesema kuwa: Licha ya kupita miaka 38 tangu
lilipotokea tukio hilo, lakini hadi leo hii hakuna hata filamu moja au
tamthilia moja au riwaya angalau moja ya kuzungumzia tukio la Tir Saba na
shahidi Beheshti na mashahidi wengine wa tukio hilo, na kama tunaona kuwa tukio
hilo limebakia hai hadi hivi sasa, jambo hilo halitokani na kitu kingine ila moyo
wa kimapinduzi wa wananchi wenyewe wa Iran.
Vile vile amegusia namna kulivyoandikwa vitabu mbali mbali kuhusiana na
operesheni za mashahidi wa kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu (vita vya
miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya mfumo
mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) na kuwataka wananchi wote
hususan vijana nchini Iran kutalii na kuvisoma kwa kina vitabu hivyo. Amesema:
Ijapokuwa kuna vitabu vingi vimeandikwa na kuhaririwa katika uwanja huo, lakini
bado wigo wa kuandika vitabu vingine vingi zaidi ni mpana sana kwa ajili ya
kuelezea vipengee na kona mbali mbali za vita vya kujihami kutakatifu na
mashahidi watukufu wa vita hivyo, kwani mienendo, matamshi na namna ya harakati
za kila shahidi ni mlango mpana wa kuingia kwenye dunia pana ya maarifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, moja ya sifa za kipekee za
kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu ni kushiriki vikosi vya kujitolea vya
wananchi vikiwa na msukumo wenye nguvu kutoka katika matabaka na daraja mbali
mbali za wananchi na kufanikiwa wananchi hao kuvitoa vita hivyo katika
kuhodhiwa na vikosi rasmi tu vya kijeshi. Amesisitiza kuwa: Nasaha zetu leo hii
pia kwa viongozi wa serikali ni kwamba wana wajibu wa kuwashirikisha vizuri wananchi
katika nyuga mbali mbali zilizopo nchini hususan uwanja wa kiuchumi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia mashahidi wa
kulinda heshima ya Ahlul Bait (Alayhimus Salaam) pamoja na mashahidi wa Haram
na kusema: Suala hilo ni katika maajabu ya kihistoria kwamba vijana wa Iran na
nchi nyingine na vijana wa nchi nyingine kutokana na imani yao thabiti na
msukumuo wao wa hali ya juu, wanasamehe maisha yao mazuri, wake zao vijana na
watoto wao wadogo na kwenda kwenye nchi nyingine ajnabi kwa ajili ya kupigana
jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na hatimaye kufa shahidi katika njia hiyo
tukufu.
Amesema, imani imara na thabiti ya mashahidi wa kulinda Haram na subira na
uvumilivu wa familia zao ni vipengee vingine vya maajabu hayo ya kihistoria na
kusisitiza kuwa: Upeo mwingine wa suala hilo, ni vile vitu vinavyoufanya imara
mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao umesimama thabiti juu ya msingi wa
imani, azma na nia ya kweli pamoja na irada ya watu waumini, wanajihadi na
mashahidi wenye imani thabiti.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, maadui wa mfumo wa
Jamhuri ya Kiislamu hawana uwezo kabisa wa kuelewa na kufahamu misingi ya
uimara na nguvu za mfumo huu wa Kiislamu na kusema kuwa: Mashahidi na familia
zao ni nguzo madhubuti kama jiwe ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na ni kwa
sababu hiyo ndio maana mfumo huu umekuwa ukifanikiwa kukabiliana na kuzishinda
changamoto za kila namna unazokabiliana nazo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kila wakati tulipoegemea kwenye
Mainduzi ya Kiislamu na moyo wa kimapinduzi, tumeweza kufanikiwa, na kila
wakati tulipojaribu kuwafurahisha mabeberu, tumeporomoka kwenye matukufu yetu
na kila wakati tulipoona muhali kutangaza misimamo yetu ya kimapinduzi kwa
uwazi, tumekuwa tukikwama na kupata hasara katika mambo yetu.
Amesisitiza kuwa, inabidi tukabiliane na mabeberu na waistikbari kwa roho ya
kimapinduzi na kuongeza kwamba: Kuwa na imani na Mwenyezi Mungu, kuwa na imani
na kushikamana na jihadi na kuwepo msukumo mkubwa wa vijana waumini na
wanapinduzi ni katika vyanzo vya nguvu na uimara wa mfumo wa Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran katika vita vyake visivyo na mlingano sawa vya kupambana na
kambi ya kiistikbari, na kwamba, licha ya mabeberu hao kuviona vyanzo hivyo vya
nguvu za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, lakini hawana uwezo wa kuvichanganua
vizuri, hivyo wanaishia kwenye kutumia mbinu za mabavu na za ukatili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, njama za mabeberu za kuunda
magenge ya kigaidi na kitakfiri kama vile Daesh ni mfano wa mbinu hizo za
kikatili na za mabavu zinazotumiwa na mabeberu katika kukabiliana na mfumo wa
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema: lengo kuu la kuanzishwa magenge hayo ya
kigaidi na kitakfiri na vitendo vyao huko Iraq na Syria lilikuwa ni kuivamia na
kuishambulia Iran, lakini nguvu za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu zimepelekea
mabeberu hao wakwame huko huko katika nchi za Iraq na Syria.
Amesema kuwa, magenge ya kigaidi na kitakfiri hayatofautishi baina ya Waislamu
wa Kishia na Kisuni na kwamba kila Muislamu anayeunga mkono Mapinduzi ya
Kiislamu na ambaye ni adui wa Marekani huwa analengwa na magenge hayo ya
kigaidi na kitakfiri. Vile vile amegusia masuala ya Bahrain na kusema: Huko
Bahrain pia tatizo la nchi hiyo si suala la Ushia na Usuni bali tatizo lake
hasa ni utawala wa madiktekta walio wachache, mabeberu na wanaojivutia kila
kitu upande wao ambao wanawakandamiza wananchi walio wengi wa nchi hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kitendo cha watawala
wa Bahrain cha kumvunjia heshima na kuchukua hatua dhidi ya alimu na mwanachuo
mwanajihadi Sheikh Isa Qasim ni ishara ya upumbavu wa viongozi hao na
kusisitiza kuwa: Sheikh Isa Qasim ni mtu ambaye alikuwa akijitihadi kadiri ya
uwezo wake kuzungumza na wananchi wa Bahrain na kuwazuia kutumia misimamo
mikali na silaha dhidi ya watawala wa nchi hiyo, lakini watawala wa Bahrain
hawajui kwamba kumvunjia heshima alimu humo mwanajihadi kuna maana ya kuondoa
kizuizi kilichokuwa kinawadhibiti vijana wenye hamasa na wenye shauku kubwa wa
Bahrain ambao wako tayari kuchukua hatua yoyote ile kukabiliana na utawala wa
nchi hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, madola ya kibeberu na vibaraka wao
mara zote wanashindwa kuwaelewa wananchi na imani ya jamii za watu hao na mara
zote wanafanya makosa katika mahesabu yao. Ameongeza kuwa: Njia sahihi ya
harakati ni kufanya harakati hizo katika njia ya Uislamu na kutawakali kwa
Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwamba ni taifa lenye imani na la watu wanajihadi na
wenye nia na azma ya kweli isiyotetereka ndilo linaloweza kuvishinda vizuizi
vyote na kusonga mbele katika mambo yake.
Ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia umuhimu wa kustafidi vizuri na kadiri
inavyowezekana na mikesha ya Laylatul Qadr katika siku hizi za mwishoni mwa
mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na kusema kuwa: Katika mikesha hiyo na nyakati
zake za usiku wa manane ambazo ni nyakati bora kabisa za tawassul na
kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu, inabidi kuomba msaada wa roho tukufu zikiwemo
roho za mashahidi na kuomba kutushufaia mbele ya Mwenyezi Mungu na
kuzihudhurisha vilivyo nyoyo zetu katika ibada ya Mwenyezi Mungu Mmoja Asiye na
mshirika na tuombe dua kwa namna ambayo Mola wetu Mtukufu atatutakabalia.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam
Walmuslimin Shahidi Mahallati, mwakilishi wa Fakihi Mtawala (Waliyyul Faqih)
ambaye pia ni mkuu wa Taasisi ya Mashahidi na Masuala ya Watu Wanaojitolea
katika Njia ya Haki, ameashiria wajibu wa kukielewesha kizazi cha vijana hamasa
na kujitolea wanamapambano wa Kiislamu katika nyakati tofauti na kusema kuwa:
Kuasisiwa na kuanza kufanya kazi sekretarieti ya Baraza Kuu la Kueneza na
Kustawisha Utamaduni wa Kujitolea na Kuwa Tayari Kufa Shahidi katika Njia ya
Haki, kuanzisha kambi maalumu ya mitandao ya Intaneti, kuimarisha na kustawisha
vyama na taasisi za watu wanaojitolea katika njia ya haki, kuanza kutekelezwa
mpango wa kuwaenzi watu wanaojitolea katika njia ya haki pamoja na kuanzishwa
kamati maalumu ya uchumi wa kimuqawama kwa shabaha ya kuongeza na kuimarisha
nguvu na uwezo wa kujitolea katika njia ya haki kwenye jamii, ni miongoni mwa
hatua na kazi kuu za taasisi hiyo ya mashahidi.