Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo katika ujumbe kwa kikao cha ishirini na nne kikuu
cha sala nchni Iran na huku akisisitizia udharura wa kila mmoja kuhisi
kuwa ana jukumu la kueneza utamaduni wa kutekeleza vilivyo ibada ya
Sala, amewataka watu wote na hususan maafisa wa taasisi husika na kila
mwenye suhula za kimaada na kimaanawi na nafasi katika uongozi, kuelewa
ukubwa na adhama ya suala hilo na kuchukua hatua za kivitendo
kulifanikisha.
Matini kamili ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu ambao umesomwa leo (Jumanne) na Ayatullah Abedini,
mwakilishi wa Kakihi Mtawala (Waliyyul Faqih) ambaye pia ni Imam wa
Ijumaa wa mkoa wa Qazvin, katika kikao kikuu cha 24 cha Sala nchini Iran
ni kama ifuatavyo:
Bismillahir Rahmanir Rahim
Ninamshukuru
Mwenyezi Mungu Mweledi wa kila kitu na Mwenye nguvu, kwa jitihada zenu
wahusika nyote wapendwa wa kusimamia na kuendesha kikao hicho muhimu, na
zaidi kwa alimu mkubwa na mujahid, janab Hujjatul Islam Bw. Qaraati,
jitihada ambazo zimezaa matunda mazuri katika sekta muhimu sana na zenye
taathira kama ambavyo zimefanya kazi nzuri pia katika kueneza faradhi
kubwa na isiyo na mbadala ya Sala.
Pamoja na hayo yote, nafasi na
medani ya kazi na vile vile mahitaji na kiu ya jamii ya Kiislamu ya
kufikia kwenye nukta inayotakiwa ni kubwa mno ikilinganishwa na mambo
yaliyopo hivi sasa. Katika ujumbe wa mwaka jana, tulionesha sehemu
fulani ya anga hiyo iliyo wazi na yenye nafasi ya kufanya juhudi za
kujazwa nafasi hizo tupu.
Ujumbe wangu wa leo utasisitizia wajibu wa
kila mtu kuhisi ana jukumu kubwa katika ufanikishaji wa jambo hilo.
Mategemeo na matarajio yangu ni kuwa, watu wote na hususan maafisa wa
taasisi husika na kila mwenye suhula za kimaada, kimaanawi na nafasi ya
uongozi, wataelewa kwa njia sahihi adhama na ukubwa wa suala hilo na
kuchukua hatua za kivitendo kulifanikisha.
Watu wote wanapaswa
kuelewa kuwa, moja ya njia muhimu na zenye taathira kubwa katika juhudi
za kupunguza matatizo na madhara katika jamii, ni kueneza utamaduni wa
Sala. Litilieni hima suala la kueneza utamaduni huo na kuhakikisha
unaenezwa kwa namna ambayo hakutakuwa na kijana wala barobaro yeyote
nchini atakayedharau Sala. Hii ni moja ya njia bora kabisa za usalama wa
kimaanawi na kiroho wa watu wetu na jamii yetu.
Vile vile lipeni
umuhimu mkubwa suala la kuhakisha watu wote wanajifunza na kujizoesha
kutekeleza ibada ya Sala kwa unyenyekevu mkuu na kuuhudhurisha moyo.
Hayo yote ni mambo yanayowezekana kufanikishwa kwa azma ya kweli ya
nyinyi wahusika wakuu na kwa kazi yenu ya kudumu na ya kuendelea katika
suala hilo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh
Sayyid Ali Khamenei
Bahman 6, 1394
(Januari 26, 2016).
3470329