IQNA

Safari ya adhana katika majimbo yote 50 ya Marekani

6:13 - May 11, 2015
Habari ID: 3284317
Jameel Syed, mwanaharakati Mwislamu wa jimbo la Michigan nchini Marekani amekamilisha safari yake ya siku 35 ya kuzunguka na kusoma adhana katika majimbo yote 50 ya nchi hiyo.

Syed ambaye kitaalmu ni afisa masoko na mwadhini katika msikiti ulioko kwenye kiunga cha Rochester katika jimbo la Michigan, alikamilisha ziara yake hiyo ya kidini siku ya Ijumaa kwa kuadhini katika msikiti huo. Jameel Syed, mwenye umri wa miaka 40 nasemekana kuwa ni mtu wa kwanza kusoma adhana katika majimbo yote 50 ya Marekani. Akizungumzia safari yake hiyo Syed amesema, ilikuwa ni safari kubwa na ya kustaajabish ambayo ilimkutanisha na Waislamu wa rangi na asili tofauti, pamoja na wasiokuwa Waislamu katika vituo vya taksi, viwanja vya ndege na misikiti. Miongoni mwa maeneo alikosoma adhana Muislamu huyo ni katika ufukwe wa Hawai ambako alikutana na kuzungumza pia na wasiokuwa Waislamu. Jameel Syed alifanya ziara pia katika msikiti wa Chapel Hill huko Carolina Kaskazini walikokuwa wakisali wanachuo watatu Waislamu waliouliwa kwa kupigwa risasi na Mzungu mmoja mapema mwaka huu. Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 10 Februari, Craig Hicks aliwaua kwa kuwapiga risasi Deah Shaddy Barakat aliyekuwa na umri wa miaka 23, mke wake Yusor Mohammad Abu-Salha, miaka 21 pamoja na dada yake Razan Mohammad Abu-Salha aliyekuwa na umri wa miaka 19 karibu na Chuo Kikuu cha Carolina Kaskazini. Japokuwa polisi ilitangaza kuwa mauaji ya wanachuo hao Waislamu yalitokana na mzozo juu ya eneo la kuegesha magari, lakini wazazi wa marehemu hao wamesema watoto hao waliuliwa kwa sababu ya chuki za kidini. Jameel Syed alikutana na familia za vijana hao wa Kiislamu na kuwapa mkono wa pole kwa msiba huo uliowafika.../mh

3278926

Kishikizo: waislamu adhana marekani
captcha