IQNA

Ban alaani hujuma ya kigaidi dhidi ya msikiti huko Kano, Nigeria

20:04 - November 29, 2014
Habari ID: 2613079
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amelaani vikali shambulizi la kigaidi kwenye Msikiti Mkuu wa Kano, Nigeria jana Ijumaa, ambalo limeripotiwa kupelekeka kuuawa watu zaidi ya 120 na kuwajeruhi wanaokisiwa kuwa mamia ya wengine.

Ban ametuma rambirambi zake kwa familia za waliopoteza maisha, pamoja na watu na serikali ya Nigeria, na kuwatakia majeruhi nafuu haraka.
Katibu Mkuu ametoa wito kwa mamlaka za Nigeria ziwafikishie haraka waliotenda uhalifu huo mbele ya mkono wa sheria, akikariri kuwa hapawezi kuwepo kisingizio chochote kinachokubalika cha kufanya mashambulizi dhidi ya raia.
Ban ameahidi uungaji mkono kikamilifu wa Umoja wa Mataifa kwa juhudi za Nigeria za kupambana na ugaidi, na kutoa ulinzi kwa raia, kwa kuzingatia sheria ya kimataifa na wajibu wa Nigeria kuhusu haki za binadamu.
Habari kutoka Kano, kaskazini mwa Nigeria zinasema kuwa, wakaazi wa mji huo wameanza kuhama makazi yao na kukimbilia katika nchi jirani ya Niger baada ya shambulizi  hilo ambalo linaaminika kutekelezwa kundi la kigaidi la Boko Haram dhidi ya msikiti mkuu mjini hapo.
Shambulizi hilo linasadikiwa kuwa ni radiamali ya Boko Haram kwa wito wa Emir wa eneo hilo, Sheikh Mohammad Sanusi, ambaye majuzi aliwataka Waislamu kukabiliana na kundi hilo la kigaidi.../mh

2612987

captcha