IQNA

Imam Khamenei aomboleza kifo cha Ayatullah Mahdavi Kani

19:58 - October 21, 2014
Habari ID: 1462701
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ametuma salamu za rambi rambi kufuatia kuaga dunia Ayatullah Mohammad-Reza Mahdavi Kani, Mkuu wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Katika salamu zake za rambi rambi kwa wananchi wa Iran, wanazuoni pamoja na familia ya mwanachuoni huyo, Kiongozi Muadhamu amesema, Ayatullah Mahdavi Kani alikuwa shujaa na sahibu wa kweli na mtiifu wa Imam Khomeini RA. Ameongeza kuwa Ayatullah Mahdavi Kani alikuwa mkweli kama mwanazuoni wa kidini, mwanasiasa na mwanamapinduzi. Aidha ameongeza kuwa mwanazuoni huyo aliyeatangulia mbele ya Haki, hakuzingatia hata kidogo masuala ya kimirengo au kikabila katika harakati zake. Ayatullah Mahdavi Kani ameaga dunia leo akiwa na umri wa miaka 84 baada ya kuugua kwa miezi kadhaa kutokana na matatizo ya moyo ambapo alikuwa amelazwa hospitalini tangu tarehe 4 Juni mwaka huu. Rais Hassan Rouhani pia ametuma salamu za rambi rambi kufuatia kuaga dunia Ayatullah Mahdavi Kani na kutangaza siku mbili za maombolezo rasmi nchini Iran.

Ayatullah Mahdavi Kani mwanazuoni mtajika hapa nchini, alikuwa miongoni mwa wanazuoni wanaharakati waliowahi kushika nyadhifa muhimu na nyeti baada ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa Iran. Marhumu Ayatullah Mahdavi Kani aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuanzia mwaka 1979-1981 katika serikali ya Mashahidi Muhammad Ali Rajai na Muhammad-Javad Bahonar. Aidha mwaka 1981 aliwahi kukaimu nafasi ya Waziri Mkuu. Katika kipindi cha uhai wake, mbali na harakati zake za kisiasa, Ayatullah Mahdavi Kani alikuwa akijishughulisha pia na kazi za kielimu ambapo alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu, Hawza na vile vile akialifu na kuandika vitabu. Viongozi mbalimbali wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu wameendelea kutoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwanazuoni huyo.../mh

1462569

 

captcha