IQNA

Jinai za Israel

Rais wa Iran amwambia Rais wa Uturuki: Kukata uhusiano wa kiuchumi na kisiasa kutaipigisha magoti Israel

10:41 - April 11, 2024
Habari ID: 3478670
IQNA-Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kukatwa uhusiano wa kiuchumi na kisiasa wa nchi za Waislamu na utawala wa Kizayuni ndiyo silaha bora ya kukomesha jinai za Wazayuni huko Palestina.

Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo jana Jumatano katika mazungumzo ya simu ya Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na sambamba na kumshukuru Rais Erdogan kwa msimamo waa nchi yake wa kulaani jinai za Israel kwenye ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus Syria amesema kuwa, jinai hiyo ya Wazayuni haitoachwa vivi hivi bila ya kupata majibu makali. Vilevile amesema kuwa, silaha kubwa zaidi ya kukabiliana na jinai za Israel huko Ghaza ni nchi zote za Waislamu kutokuwa na uhusiano wowote na utawala wa Kizayuni.

Rais Raisi amelalamikia pia uungaji mkono wa Marekani na madola ya Magharibi kwa Israel na udhaifu wa kupindukia wa vyombo vya kimataifa mbele ya jinai za Wazayuni akisisitiza kuwa, mambo hayo ndiyo yanayoufanya utawala wa Kizayuni kuwa na kiburi na kutojali.

Kwa upande wake, Rais Erdogan wa Uturuki amesema kwenye mazungumzo hayo ya simu kwamba nchi yake inalaani shambulio la utawala wa Kizayuni katika ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus Syria na kusisitiza kuwa, leo hii utawala wa Kizayuni wa Israel umetengwa mno na unachukiwa zaidi duniani kuliko wakati mwingine wowote. 

Tangu tarehe 7 Oktoba 2023 hadi hivi sasa utawala wa Kizayuni unafanya jinai za kutisha dhidi ya wanawake, watoto wadogo na raia wa kawaida kwenye Ukanda wa Ghaza huko Palestina mbele ya kimya ya jamii ya kimataifa na msaada wa pande zote wa madola ya kibeberu.

4209882

captcha