IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Chuo cha Kidini (Hawza) Iran ni cha kimapinduzi

19:54 - March 15, 2016
Habari ID: 3470198
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Chuo cha kidini (Hawza) mjini Qum kinapaswa kubakia "Chuo cha Kimapinduzi na Chimbuko la Mapinduzi" na ili kufikia lengo hilo kuna haja ya kuwepo fikra, tadbiri na mpango wa kina."

Ayatullahil Udhma Khamenei ameyasema hayo leo katika mkutano wa wanachama wa jumuya ya wawakilishi wa wanachuo na wanazuoni wa Hawza ya mji mtakatifu wa Qum (kusini mwa Tehran). Amefafanua kuhusu nafasi ya kipekee na yenye taathira ya Hawza ya Qum katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kuwepo njama za baadhi kwa lengo la kuondoa utambulisho wa kimapinduzi wa vyuo vya kidini na kusema: "Vyuo vikuu na vyuo vya kidini vimekuwa na taathira ya wazi katika kuibuka na hatimaye kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu."

Ayatullah Khamenei amesema kuwepo taathira katika harakati na mapambano ya wanachuo wa vyuo vikuu katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kutokana na kuwepo wahusika wakuu yaani mapambano ya maulamaa wa Kiislamu. Ameongeza kuwa: "Mapambano ya wanafunzi wa vyuo vikuu kwa yakini yangeishia katika kuta za vyuo vikuu kama si kushiriki maulamaa wa Kiislamu katika mapambano."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: 'Upana na taathira' ni sifa mbili za harakati ya maulamaa katika Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: "Hawza ya Qum ina sehemu mbili ambazo ni 'Marjaiya na Wanachuo' ambapo Imam Khomeini RA akiwa katika sehemu ya Marjaiya alikuwa akitoa taarifa na hotuba huku hotuba na mitazamo ya Imam MA, ikifikishwa katika kina cha jamii na katika maeneo ya mbali zaidi kupitia wanazuoni na wanachuo wa vyuo vya kidini.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, kama Hawza ya Qum haingekuwepo, pengne harakati ya Imam Khomeini MA haingefanikiwa na jambo hilo linaonyesha nafasi muhimu ya Hawza ya Qum katika kuibuka na kuendelea Mapinduzi ya Kiislamu.

3483511

captcha