IQNA

Shekhe Mkuu wa Al Azhar asisitiza Umoja wa Kiislamu

15:03 - August 25, 2015
Habari ID: 3351450
Shekhe Mkuu wa Al Azhar Sheikh Ahmed el-Tayeb amesisitiza kuhusu umuhimu wa kudumisha umoja wa Kiislamu.

Katika jawabu lake kwa barua ya mwanachuoni mwandamizi na mmoja kati ya marajii Taqlid wa Mashia Ayatullah Nasser Makarem Shirazi wa Iran, Sheikh el-Tayeb amesema Mashia na Masuni hawafaidiki na mizozo ya kimadhehebu. Ameongeza kuwa ni maadui wa Uislamu tu ndio hunufaika na migongano baina ya Waislamu.
Mwanazuoni huyo mwandamizi wa Masuni amesisitiza kuhusu mazungumzo baina ya madhehebu ya Kiislamu na kusema, "Daima nimekuwa nikisisitiza kuhusu umuhimu wa kuwepo kongamano litakalowaleta pamoja wanachuoni wa madhehebu ya Shia na Suni ili kukabiliana na njama dhidi ya Umma wa Waislamu."
Aidha Shekhe huyo mkuu wa Al Azhar nchini Misri amesema maulamaa wanapaswa kutoa Fatwa dhidi ya wakufurushaji au matakfiri na wale wanaowaua Waislamu na watu wengine wasio na hatia.
Katika barua yake kwa Sheikh el-Tayeb wiki chache zilizopita, Ayatullah Makarem Shirazi alisema madhehebu ya Shia na Suni ni mabawa mawili ya Umma wa Kiislamu huku akisisitiza kuwa migogoro ya kimadhehebu inatokana na njama zinazoibuliwa na maadui wa Uislamu.../mh

3351293

captcha