IQNA

Jinai za Israel

Al Azhar yatangaza mashikamano na Wapalestina, yalaani jinai za Israel

10:53 - December 01, 2022
Habari ID: 3476177
TEHRAN (IQNA)- Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar nchini Misri kwa mara nyingine tena kimeutaka ulimwengu uzingatia katika machungu na mateso ya taifa la Palestina na kukaliwa kwa mabavu ardhi sambamba na kulaani jinai za umwagaji damu zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi Wapalestina.

Al-Azhar ilitoa taarifa hii kali dhidi ya Uzayuni kwa mnasaba wa  kumbukumbu mbaya zaidi ya historia ya kisasa ambayo ni kumbukumbu ya kugawanywa kwa Palestina. Siku ambayo inasadifiana na Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Taifa la Palestina, ambayo ni Novemba. 29 kila mwaka.
Kwa mujibu wa tovuti ya "Rai Al Youm", katika mnasaba huu, Al-Azhar kwa mara nyingine tena imesisitiza azma yake ya kudumu ya kuliunga mkono taifa la Palestina na mapambano yake ya kisheria na halali ya ukombozi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel. Aidha Al Azhar imetangaza upinzani wake kamili njama zote za Wazayuni za Uyahudishaji ambazo zinafanyika  kwa lengo la kutaka kubadilisha utambulisho, na muundo wa idadi ya watu wa Palestina na kunyakua ardhi zao zote.


Katika kauli hiyo, Al-Azhar imesisitiza kwamba vitendo hivyo vya Wazayuni vinaonyesha utambulisho halisi wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ni utamblisho wa umwagaji damu na ukatili. 
Katika taarifa hiyo inasisitizwa kuwa, mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kamwe hayatasahau ukatili, mauaji ya halaiki na jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya taifa la Palestina.

Al Azhar imesema uhalifu huo hauwezi kufutika katika kumbukumbu za ubinadamu hata kamai utawala wa Kizayuniunajaribu kupotosha historia.

Wakati huo huo, Rais wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar cha Misri amesisitiza uungwaji mkono kamili wa chuo hicho kwa ajili ya Palestina.

Akihutubia katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Wananchi wa Palestina siku ya Jumanne, Sheikh Salama Daoud alilaani hatua za utawala wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa.

Amesema wanaounga mkono na kusaidia ukiukaji huo ni washirika wa ukatili dhidi ya watu wa Palestina.

Sheikh Daoud ameongeza kuwa, Al-Azhar itaendelea kuunga mkono mapambano ya wananchi wa Palestina kwa ajili ya kuanzisha taifa huru la Palestina huku mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem) ukiwa ni mji mkuu wake.

Amesema mshikamano na Wapalestina wanaodhulumiwa na kusimama nao dhidi ya madhalimu ni wajibu wa kila binadamu mtukufu anayependa uadilifu na kuchukia dhulma.

Al-Azhar inaiomba jumuiya ya kimataifa  kusimama pamoja na taifa la Palestina na kuunga mkono mapambano yake halali dhidi ya utawala dhalimu wa Kizayuni na vitendo vyake vya kigaidi.
Ikumbukwe kuwa, mwaka 1977 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza Tarehe 29 Novemba kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Taifa la Palestina. Sababu ya hatua huyo ya Umoja wa Mataifa ni nafasi na mchango wa Baraza Kuu la umoja huo katika kuigawa ardhi ya Palestina. 

4103561

Habari zinazohusiana
captcha