IQNA

Shakhsia katika Qur'ani/9

Adhabu ya Kwanza ya Mwenyezi Mungu: Gharika ya Nuhu

18:37 - October 05, 2022
Habari ID: 3475884
TEHRAN (IQNA) – Katika historia, adhabu mbalimbali zimetumwa na Mwenyezi Mungu kwa wale waliofanya madhambi makubwa. Adhabu ya kwanza kati ya hizo ilikuwa gharika iliyokuja wakati Nuhu (AS) alipokuwa Nabii wa Mwenyezi Mungu.

Wakati wa mafuriko hayo, wale ambao hawakuamini katika mwongozo wa manabii wa Mwenyezi Mungu waliangamia.

Nuhu (AS) alikuwa wa kwanza kati ya Mitume watano wa Ulul-Aadham. Kulingana baadhi ya riwaya, Nuhu alitoka katika kizazi cha tisa cha watoto wa Adamu. Kuna maelezo tofauti kuhusu wakati wake wa kuzaliwa. Vyanzo vingine vinasema alizaliwa Adamu alipokufa. Kuhusu mahali alipoishi, wengine wanaamini kwamba aliishi Mesopotamia na mahali ambapo sasa ni Kufa huko Iraq.

Miongoni mwa sifa za Nuhu ni kushukuru kwa baraka za Mwenyezi Mungu.

Yeye ni baba wa ubinadamu na mbali na Adam, Shayth na Idris, mitume wengine wote wa Mungu walikuwa kizazi chake.

Mke wake Nuhu alikuwa Waliya na alikuwa na wana wanne: Saam, Ham, Yaafth na Kanaan.

Baada ya kifo cha Adam, watu walikuwa Ummah mmoja na wote walikuwa ni wenye kumuabudu Mungu Mmoja. Walikuwa na maisha rahisi na ya kawaida. Hatahivyo Baada ya muda baadhi yao walianza kukengeuka kutoka kwenye njia ya uwongofu. Ibada ya masanamu na ushirikina zilipoenea, Mwenyezi Mungu alimtuma Nuhu kwa watu kama nabii. Alitumia miaka 950 kuwaalika watu wake kwenye njia ya haki ya Tauhidi ya kumuabudu Mungu Mmoja na kuacha ibada ya masanamu. Hata hivyo, hakuna aliyeamini ila wachache. Hapo ndipo Nuhu alipopewa jukumu la kujenga Safina.

Inasemekana kuwa kazi ya Nuhu ilikuwa useremala. Ingawa alikuwa mahiri katika useremala, kujenga chombo kusafiri katika maji kwa amri ya Mungu ilikuwa inafanyika kwa mara ya kwanza. Na akaanza kuijenga mahali palipokuwa mbali na maji. Ndiyo maana watu ambao hawakuamini ujumbe wa Nuhu walianza kumdhihaki. Miongoni mwao alikuwemo mkewe na mwanawe Kanaani.

Baada ya Safina kukamilika, Nuhu, kwa amri ya Mungu, aliiagiza familia yake na wale waliomwamini kupanda chomboni. Pia alichukua wanyama pamoja naye wawili wawili.

Kisha ghafla dhoruba kubwa ikatokea na baadaye kukatokea mafuriko makubwa. Ni wale tu waliomwamini Nuhu na kupanda Safina ndio waliosalimika. Wengine wote, akiwemo mwanawe Kanaan, walipoteza maisha.

Baada ya muda fulani adhabu ya hiyo kutoka kwa Mwenyezi Mungu iliisha na Safina ikatua kwenye Mlima Judi (au Cudi), ambao uko kusini-mashariki mwa Uturuki.

Kwa hiyo Nuhu alikuwa nabii wa kwanza ambaye katika zama zake kulikuwa na adhabu ya moja kwa moja kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Hakuna ripoti kuhusu maisha ya Nuhu baada ya gharika. Inaripotiwa tu kwamba aliishi miaka 60 au 79 baada ya hapo. Kwa jumla, inasemekana aliishi kati ya miaka 930 hadi 2,500.

Kwa mujibu wa baadhi ya maelezo, kaburi lake liko Najaf, Iraq, kando ya kaburi tukufu la Imam Ali (AS) ingawa baadhi ya ripoti nyingine zinasema alizikwa Makka , Mosul au Kufa nchini Iraq, India, Lebanon au Iran.

Kishikizo: nuhu nabii safina gharika
captcha