IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran vilikuwa ni matokeo sera za mfumo wa kibeberu

21:59 - September 21, 2022
Habari ID: 3475816
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran vilikuwa ni matokeo ya siasa za kimkakati za mfumo wa kibeberu katika uadui wake dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema leo mjini Tehran hayo katika hafla ya kuwaenzi maveterani wa vita vya kujihami kutakatifu na kubainisha kwamba, licha ya kuweko himaya na uungaji mkono wa kila upande wa madola makubwa ya ulimwengu kwa Saddam dikteta mpenda jaha na mwendawazimu wa madaraka, lakini vita hivyo viliondoka katika hali ya kuwa tishio na kubadilika na kuwa fursa.

Kiongozi Muadhamu amevitaja vita vya kutwishwa Iran na Iraq kuwa tukio lililojaa hamasa, maana kubwa na faida lukuki kwa ajili ya leo na kesho ya nchi hii ambapo sambamba na kuashiria nyaraka zilizotolewa na madola ya Magharibi kuhusiana na vita hivyo amesema, kutishwa Iran vita ilikuwa radiamali ya kawaida ya madola ya kibeberu duniani kwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran haukuwa pigo kwa mfumo tegemezi na fisadi na dhoruba kwa Marekani na uistikbari tu, bali mapinduzi hayo yalikuwa tishio kwa mfumo wa kibeberu; na ni kutokana na waistikbari wa magharibi na mashariki kudiriki tiishio hilo ndio maana wakamshawishi na kumchochea dikteta Saddam aanzishe vita dhidi ya Iran.

Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, kudhihiri na kuibuka mfumo wa kisiasa wenye kujitegemea, tena katika taifa ambalo lilikuwa nukta ya matumaini, tegemeo na uchu wa Marekani, ni jambo ambalo halikuwa likivumilika kwa Marekani na mabeberu, na ndio maana baada ya kushindwa kufikia malengo yao katika njama chafu kama za mapinduzi, shambulio la Tabas na uchochezi wa kikaumu wahusika waliamua kuanzisha vita vya kila upande dhidi ya Iran.

4086952

captcha