IQNA

Uislamu na teknolojia

Metaverse ya kwanza ya Kiislamu duniani

15:56 - May 22, 2022
Habari ID: 3475282
TEHRAN (IQNA)- Shirika moja la masuala ya uchumi wa Kiislamu limetangaza kuzindua Metaverse ya kwanza ya Kiislamu ambayo inaenda sambamba na mafundisho ya Kiislamu.

Shirika la IBF.NET limesema limesema litapanua shughuli zake za kiuchumi mitandaoni kwa kuzindua metaverse aina mbili, moja ya masomo na nyingine itakuwa ni soko.

Wazo la metaverse ya Kiislamu liliwasilishwa kwa mara ya kwanza katika makala iliyotumwa katika blogu ya IBF NET na baadaye mchakato wa utekelezaji wake ukaanza.

Je, metaverse ni nini?  Kwa kifupi ni kuwa, metaverse ni ulimwengu mpya wa kidijitali ambao watu wanaweza kuishi pamoja kwa njia ya intaneti. Maana yake ni kuwa, ni ulimwengu wa kidijitali na kwa msingi huo haupo katika mazingira ya kweli, upo katika mtandao.

Weledi wa masuala ya teknolojia wanasema metaverse ni hatua inayofata ya ustawi wa intaneti na teknolojia hii inajumuisha ile teknolojia inayojulikana kama uhalisia ulioigwa (Virtual Reality au VR).

Badala ya kuwa katika kompyuta , watu katika metaverse watatumia headset kuingia ulimwengu usio halisi na kuunganishwa katika mazingira yote ya kidijitali.

Inatumainiwa kwamba ulimwengu usio halisi wa VR huenda ukatumika kwa chochote kuanzia kufanya kazi, kucheza michezo pamoja na kujiunga na matamasha hadi kuwasiliana na marafiki na familia.

Hata shirika la Facebook limeshabadilisha jina lake la kampuni na kujiita Meta ikiwa ni mpango wake wa kujiimarisha kuelekea katika ulimwengu mpya wa kidijitali.

Mmimiliki wa Facebook Mark Zuckerberg alitangaza jina hilo jipya wakati alipokua akizindua mipango ya kujenga "metaverse" - ulimwengu wa mtandao ambapo watu wanaweza kushiriki katika michezo, kufanya kazi , kuwasiliana katika mazingira yalioigwa na yasio na uhalisi kwa kutumia vitoa sauti vinavyovaliwa katika kichwa  au headset.

Kwa kuzingatia teknolojia hii mpya ibuka, kuna haja ya kuwa na mitandao yenye kutoa huduma kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu. Ni kwa msingi huo ndio shirika la IBF NET likazindua metaverse ya Kiislamu kuwahudumia Waslamu zaidi ya bilioni mbili kote duniani. Inatazamiwa kuwa mashirika mengine ya Kiislamu katika uga wa teknolojia yataiga mfano huo na kutoa huduma hii muhimu hasa kwa vijana ili wasipotoshwe na mitando mingine isiyozingatia maadili na mafundisho ya kidini.

Kwa mujibu wa Mohammad Alim, Mkurugenzi wa IBF NET, mradi wa metaverse wa shirika hilo unalenga kufungua kituo cha masomo ambapo washiriki wataweza kusoma na kubadilisha mawazo ya kieleimu popote pale na wakati wowote ule na pili ni kufungua soko la kuuza na kunua bidhaa na yote hayo yatafanyika kwa kuzingatia maadili ya Kiislamu.

Aidha anasema wanalenga kufafanua namna teknolojia ya metaverse ilivyo na manufaa kwa jamii za Waislamu na ni kwa msingi huo wanasisitiza kuwa lazima maadili ya Kiislamu yazingatiwe.

4058636

captcha