Tayari waumini wamemiminika katika Haram ya Imam Hussein AS kwa ajili ya Siku ya Arubaini.
Maadhimisho siku ya Arubaini (Arobaini au Arbaeen) hufanyika kila mwaka tarehe 20 Safar, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria, baada ya kupita siku Arobaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram, kwa ajili ya kukumbuka siku aliyouawa shahidi mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein AS na masahaba zake ambao walijitolea roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika jangwa la Karbala mwaka 61 Hijria Qamaria. Haram Takatifu ya Imam Hussein AS iko katika mji huo wa Karbala.
Mamilioni ya watu wa Iraq hutembea kwa miguu kutoka miji yao ya mbali na karibu ili kufika Karbala katika siku hiyo ya Arubaini. Halikadhalika wafanyaziara kutoka nchi mbali mbali hushiriki kwa mamilioni katika hafla hiyo. Mwaka huu kutokana na vizingiti vya corona idadi ya washiriki wa Arubaini inatazamiwa kupungua. Siku ya Arubaini ambayo mwaka huu intazamiwa kusadifiana na Septemba 27.