IQNA

Sayyed Ebrahim Raeisi achaguliwa kuwa rais mpya wa Iran

19:09 - June 19, 2021
Habari ID: 3474022
TEHRAN (IQNA)- Baada ya kumalizika zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran imetangaza matokeo rasmi ya uchaguzi huo ulioshirikisha mamilioni ya wapiga kura.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abdolreza Rahmani Fazli ametangaza matokeo hayo leo Jumamosi mbele ya waandishi wa habari hapa jijini Tehran na kusema kuwa, wapiga kura milioni 28 na laki tisa na 36 elfu na nne wameshiriki katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amesema, asilimia 48.8  ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura wameshiriki kwenye uchaguzi huo. Ameongeza kuwa, Sayyid Ebrahim Raeisi ndiye aliyechaguliwa kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kura milioni 17 na laki 9 na 25,345 za wananchi.

Waziri huyo wa Mambo ya Ndani wa Iran pia amesema, Mohsen Rezaei amepata kura milioni 3 na laki nne na 12,712, Abdel Naser Hemmati amepata kura milioni 2 na laki nne na 27,201 na Sayyid Amir Hossein Qazizadeh Hasheimi amepata kura laki 9 na 99,718.

Uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uchaguzi wa sita wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji ulifanyika jana Ijumaa tarehe 18 Juni, 2021. Hiyo hiyo jana kulifanyika pia uchaguzi wa kwanza mdogo wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Kiislamu na uchaguzi wa pili mdogo wa Baraza la Tano la Wanachuoni Wataalamu wanaomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Zoezi la kupiga kura lilimalizika Jumamosi (Juni 19) saa nane usiku, masaa 19 baada ya vituo vya kupigia kura kufunguliwa saa moja asubuhi Ijumaa, Juni 18.

Muda wa zoezi la kupiga kura uliongezwa mara kadhaa ili kuhudumia idadi kubwa ya wapiga kura na pia kutokana na uzingatiaji wa kanuni za kiafya za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Zaidi ya Wairani milioni 59 walikuwa wametimiza masharti ya kupiga kura katika uchaguzi ambao ulikuwa wa wagombea wanne baada ya Wagombea wengine watatu kujiondoa katika mchuano huo Jumatano.

Jana pia kulifanyika uchaguzi wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji na halikadhalika uchaguzi mdogo wa bunge na baraza la wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu.

3978679

captcha