IQNA

Mwanariadha Muislamu Marekani apigwa marufuku kwa sababu ya kuvaa Hijabu

19:06 - October 26, 2019
Habari ID: 3472188
TEHRAN (IQNA) – Msichana Muislamu nchini Marekani ameondolewa kwenye mashindano ya mbio za nyika kwa sababu ya kuvaa Hijabu.

Noor Alexandria Abukaram mwenye umri wa miaka 16 amelaani vikali udhalilishaji na ubaguzi aliofanyiwa kwa misingi ya dini yake wakati wa mashindano ya mbio za nyika katika mji wa Findlay jimboni Ohio mapema mwezi huu.

Mwanafunzi huyo wa shule ya upili ya Sylvania Northview amesema, "Moyo wangu ulivunjika baada ya kuambiwa kuwa nimeondolewa kwenye mashindano hayo muhimu eti kwa kuwa nilikuwa nimevaa hijabu, vazi ambalo eti linakiuka mavazi ya michezo yaliyoanishwa."

Amesema alishangazwa na uamuzi huo wa ghafla kwa kuwa amekuwa akivalia vazi hilo la staha siku zote na anasisitiza kuwa, hijabu ni sehemu ya mwili wake na maisha yake.

Mama yake Noor Alexandria Abukaram , Bi Yolanda Melendez amesema binti yake amekuwa akishiriki katika riadha bila matatizo nah ii ni mara ya kwanza kupigwa marufuku. Wakati huo huo Seneta Elizabeth Warren wa Massachusetts, ambaye anawania kugombea urais kwa tikiti ya chama cha Democrat, amemuunga mkono Abukaram huku akikosoa ubaguzi kwa msingi wa dini. Amesema wanafunzi Waislamu wanapaswa kuhisi wanakaribishwa shuleni na hawapaswi kuzuiwa kushiriki katika shughuli zozote shuleni kwa sababu ya kuamua kuvaa Hijabu. Hii ni katika hali ambayo, mwezi uliopita, binti mwingine wa Kiislamu ambaye anachezea timu ya taifa ya mchezo wa squash ya Marekani aliwafungulia mashitaka wafanyakazi wa shirika la ndege la Air Canada kwa kumlazimisha kuvua hijabu kabla ya kuabiri ndege ya shirika hilo nchini Marekani.

Hivi karibuni pia, askari Mwislamu wa kike katika jeshi la Marekani kwa jina Cesilia Valdovinos aliwafungulia mashtaka makamanda wake kwa kumlazimisha kuvua hijabu.

Baraza la Uhusiano wa Kiislamu nchini Marekani (CAIR) limeonya kuwa vitendo vya uhalifu vinavyotokana na chuki dhidi ya Uislamu vimeongezeka nchini humo haswa tangu Donald Trump alipoingia madarakani nchini humo.

3469740

captcha