IQNA

Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran inakaribia makabiliano ya pande zote na adui

12:23 - May 17, 2019
Habari ID: 3471961
TEHRAN (IQNA) - Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC), amesisitiza kwamba maadui wamefikia mwisho wa njia na kwamba licha ya haiba yao ya kidhahiri lakini mifupa yao imeoza kwa ndani.

Iran inakaribia makabiliano ya pande zote na adui

Akizungumza katika uzinduzi wa mfumo mkubwa zaidi wa jihadi mjini Tehran, Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribia ukingo wa makabiliano ya pande zote na adui. Amesema maadui wanajaribi kusambaratisha mapambano na muqawama wa wananchi wa Iran kupitia mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi kwa kutumia uwezo wao wote. Hatahivyo amesema, kwa mara nyingine maadui watashindwa katika njama zao.

Akihutubu katika kikao hicho siku ya Jumatano, Meja Jenerali Salami aliongeza kuwa:  “ Hii leo maadui wanatumia mbinu ya 'mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi' na kuleta uwezo wao wote (zana za kivita) katika medani kwa lengo la kudhoofisha na kuushinda ukakamavu wa taifa la Iran, lakini wameghafilika na ukweli huu kwamba utulivu, usalama, heshima na utukufu wa Iran unatokana na mapambano, kusimama imara pamoja na subira, na bila shaka maadui watashindwa katika uwanja huu.”

Uadui na chuki ya Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran imefikia kilele ikiwa ni mwaka mmoja baada ya nchi hiyo kujiondoa katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia mashuhuri kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA. Kwa kutumia 'mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi' sambamba na vitisho vya kijeshi, Marekani inataka kuilazimisha Iran isalimu amri na kukubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo kwa masharti yake (Marekani).

Lengo la serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani na timu yake ya mashinikizo na vita ni kuanzishwa mazungumzo mapya ambayo licha ya kujadili masuala ya nyuklia yatajumuisha pia uwezo wa makombora wa Iran na ushawishi wake chanya katika eneo na Asia Magharibi (Mashariki ya Kati). Trump aliiondoa Marekani katika mapatano ya JCPOA tarehe 8 Mei mwaka jana kwa kisingizio kwamba yalikuwa na kasoro na kuwa hayakujumuisha kila masuala yanayohusiana na Iran. Ili kufikia ndoto hiyo ambayo kamwe haitathibiti, Marekani imekuwa ikishirikiana kwa karibu na utawala haramu wa Israel pamoja na tawala vibaraka za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi. Kuitaja Iran kuwa ni tishio katika eneo hili, kumegeuzwa na serikali ay Trump kuwa kisingizio kizuri cha kuendelea kuzikamua tawala hizo vibaraka.

 Ushirikiano wa kisiasa unaofanywa na baadhi ya nchi za Kiarabu na hasa Saudi Arabia na serikali ya Trump unatekelezwa kwa lengo moja tu, nalo ni la kuwa katika kambi moja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ni katika hali ambayo kambi hiyo tayari imeshindwa na mrengo wa mapambano ukiongozwa na Iran katika medani za vita huko Syria, Iraq na Yemen. Nguvu na ushawishi chanya wa Iran katika eneo la Asia Magharibi na mambo yanayopelekea kuimarika kwa nguvu hiyo yakiwemo makombora, ni suala ambalo limeikasirisha sana Marekani na vibaraka wake katika eneo. Siku hizi, kuongezeka kwa hujuma ya kipropaganda dhidi ya Iran kimsingi ni vita vya kisaikolojia tu, na ni wazi kuwa siasa hizo za Marekani hazitaifanya Iran iwachane na mambo hayo yanayopelekea kuimarika kwa nguvu na ushawishi wake katika eneo.

3812012

captcha