IQNA

Taasisi ya Darul Iftaa ya Misri

Mchezo wa Video wa ‘Blue Whale’ ni Haramu katika Uislamu

13:01 - April 08, 2018
Habari ID: 3471458
TEHRAN (IQNA)- Taasisi ya Darul Iftaa ya Misri, ambayo hutoa muongozo wa Kiislamu nchini humo, imetangaza kuwa mchezo maarufu wa video wa ‘Blue Whale’ ni haramu katika Uislamu baada ya kubainika kuwa watu kadhaa walioucheza wameishia kujitoa uhai.

Darul Iftaa imetangaza uamuzi huo baada ya kijana wa Kimisri mwenye umri wa miaka 18 kujitoa uhai baada ya kucheza mchezo huo wiki iliyopita.

Katika taarifa, Darul Iftaa imesema mchezo huo una nukta kadhaa ambazo ni haramu kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu. Mwakilishi wa Darul Iftaa amesema mchezo huo huwashurutisha wanaocheza kutekeleza vitendo vya kujiduhuru kama mojawapo ya changamoto na hatimaye humshajiisha mchezaji kujiua. “Baada ya kufanya uchunguzi na utafiti kuhusu mchezo huu, tumefikia natija kuwa ni mchezo mchafu ambao unaleta madhara na kwa msingi huo ni haramu kuucheza. Tunatoa wito kwa vijana wetu kutumia wakati wao wakifanya kazi ambazo zinamanufaa kwao binafsi na kwa jamii nzima.

Kifo cha mtoto wa mbunge wa zamani Misri kimewashtua wengi Misri baada ya familia kusema alijiua baada ya kucheza mchezo huo wenye utata. Familia yake imesema alijitia kitanzi akiwa katika chumba chake ambacho kilikuwa kimechorwa nembo ya mchezo wa video wa Blue Whale.

Mwaka jana, Bodi ya Kuanisha Filamu Kenya (KFCB) nayo pia ilipiga marufuku mchezo wa video wa ‘Blue Whale’ baada ya vifo kuripotiwa nchini humo.

“Tumepata habari kuhusiana na mchezo wa mtandao ambao unatumiwa kuwafanya watoto kutekeleza hatua hatari kupitia kwa michezo ya siku 50 mfululizo,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa KFCB Dkt Ezekiel Mutua.

Michezo ambayo imejumuishwa katika ‘Blue Whale’ ni pamoja na kutazama video ya kutisha na kujidhuru.

Sehemu ya mwisho ya mchezo huo ‘The Blue Whale Challenge’ hushinikiza mchezaji kujitoa uhai ili aweze kuwa ‘mshindi’.

Mchezo huo unahusiana na michezo mingine kama vile ‘A Silent House’, ‘A Sea of Whale’, ‘Wake Me Up at 2.40am’, alisema Dkt Mutua, na hulenga watoto na vijana wa umri mdogo.

Kwa mujibu wa rasimu ya orodha ya mwaka 2018 ya magonjwa iliyotayarishwa na WHO, utumizi wa kupindukia wa michezo ya video na kompyuta unatambuliwa kama aina moja ya uraibu.

Wataalamu wanasema iwapo michezo hiyo ya kidijitali itapewa umuhimu na kipaumbele kuliko shughuli zingine za kawaida za kimaisha basi huo unaweza kutajwa kuwa ni uraibu unaohitajia matibabu.

3465503

captcha