IQNA

Mkuu wa Hamas amuandikia barua Kiongozi Muadhamu akipongeza sera za Iran kuhusu Quds

22:11 - January 19, 2018
Habari ID: 3471361
TEHRAN (IQNA) Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amemuandikia barua Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akishukuru na kupongeza sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu Quds Tukufu.

Ismail Hania amesema katika barua hiyo kwamba: "Wananchi wote wasiotetereka wa Palestina wanaithamini misimamo imara na yenye thamani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na kadhia ya Palestina, Quds pamoja na uungaji mkono kwa mapambano ya wananachi wa Palestina bila kusahau misaada yake mbalimbali kwa taifa la Palestina."

Kiongozi huyo wa Hamas amesisitiza pia katika barua yake hiyo kwamba: "Hapana shaka kuwa, kwa miongozo ya Kiongozi Muadhamu, Iran imekuwa na itaendelea kuwa juu zaidi katika kuwaimarisha mujahidina na wanapambano na kulifanya chaguo la muqawama na mapambano kujikita zaidi Palestina."

Akiashiria njama za Marekani na Wazayuni za kuibua chuki ya Sunni na Shia, Ismail Haniya amesema: Marekani na baadhi ya watawala walioshindwa wanataka kulifutilia mbali suala la Palestina na mapambano dhidi ya utawala vamizi wa Israel ili viongozi ambao wanapiga ngoma ya kuiridhisha Marekani na Israel wapate fursa ya kudhihirisha wazi uhusiano wao na Israel; na mkabala na hilo, kwa kuelekeza uadui upande wa Iran sambamba na kuchochea chuki na taasubi za Kishia na Kisuni waikengeushe dira ya Umma wa Kiislamu.

Ismail Haniya amesisitiza kuwa, Quds Tukufu ni mji mkuu wa kisiasa wa taifa la Palestina na pia ni mji mkuu wa kidini wa Waislamu na wapenda haki kote duniani.

Kadhalika ameashiria kile alichokitaja kama 'njama kuu' ya madola ya kibeberu dhidi ya Quds na Wapalestina, akisisitiza kuwa njama hizo za maadui zinalenga kuusambaratisha Ukanda wa Gaza, ambalo ni shina la muqawama na kuzima mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ili hatimaye wafanye kuwa wa kawaida uhusiano wa Israel na tawala vikaragosi za eneo hili.

Itakumbukwa kuwa, Disemba sita mwaka jana, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa eti Quds ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, hatua ambayo imeendelea kulaaniwa kimataifa

3683108

captcha